KOCHA Mkuu wa Simba, Mhispania, Franco Pablo, ameweka rekodi ya kucheza michezo mitatu mfululizo ya Ligi Kuu Bara, sawa na dakika 270 bila ya kupata bao katika msimu huu.
Kocha huyo aliyebeba Kombe la Mapinduzi, ameweka rekodi hiyo tangu ajiunge na timu hiyo msimu huu akichukua nafasi ya Didier Gomes aliyesitishiwa mkataba.
Simba msimu huu inaonekana ni butu kwenye ushambuliaji, ikiwa kwa ujumla haijafunga bao lolote katika mechi sita za ligi kati ya 13 ilizocheza hadi sasa.
Timu hiyo iliyorejea juzi ikitokea mkoani Bukoba kucheza dhidi ya Kagera Sugar mchezo wa ligi, keshokutwa Jumapili inatarajiwa kuvaana na Dar City kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC).
Katika mechi hizi tatu mfululizo ambazo Simba haijapata bao lolote, ni dhidi ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya ambao walifunga 1-0, aliyewaliza akiwa ni Paul Nonga.
wake wa pili ni dhidi ya Mtibwa Sugar uliomalizika kwa suluhu kwenye Uwanja wa Manungu, kisha Jumatano pale Kaitaba, Bukoba wakachapwa 1-0, bao likifungwa na Mganda, Hamis Kiiza ‘Diego’.
Katika mchezo huo dhidi ya Kagera, Pablo aliwaweka benchi washambuliaji wote huku akitumia viungo pekee katika safu ya ushambuliaji huku Mghana, Bernard Morrison akimpanga namba tisa.
Morrison tangu ajiunge na timu hiyo katika msimu uliopita akitokea Yanga, hajawahi kucheza nafasi hiyo ya ushambuliaji lakini Jumatano alipangwa.