Pablo apongeza wachezaji Simba




LICHA ya kuambulia sare juzi dhidi ya Mtibwa Sugar, Kocha Mkuu wa Simba, Pablo Franco amesema wachezaji wake wamepambana na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga, lakini bahati haikuwa kwao kupata ushindi katika mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania uliopigwa Uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro.

Akizungumza na gazeti hili jana, Pablo alisema licha ya kutoka sare ya bila kufungana dhidi katika mchezo huo, ana kila sababu ya kuwapongeza wachezaji wake kwa namna walivyojituma.

Alisema ingawa uwanja haukuwa rafiki kwa wachezaji wake na aina ya soka linalochezwa na timu hiyo, lakini walipambana muda wote kutafuta ushindi.

“Ingawa tumecheza vizuri na wachezaji kupambana muda wote kuhakikisha tunapata ushindi, naamini haikuwa bahati kwetu kuondoka na pointi zote tatu,” alisema Pablo.

Alisema walitengeneza nafasi nyingi kipindi cha pili ambazo wangeweza kuzitumia na kupata mabao kama nafasi ya dakika ya mwisho ya Shomari Kapombe.

“Pamoja na uwanja haukuwa rafiki kwa wachezaji na aina ya soka tunalocheza, lakini tulipambana muda wote kutafuta ushindi, nimependa jinsi walivyojituma, tumekuwa tukicheza mechi karibu karibu, wachezaji wanaumia hakuna jinsi tunapaswa kucheza na tunarudi Dar es Salaam, tutapata siku moja ya mazoezi kabla ya kwenda Kagera,” alisema Pablo.

Simba itashuka tena dimbani Jumatano kuvaana na Kagera Sugar kwenye mechi yao ya kiporo itakayopigwa katika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad