KOCHA Mkuu wa Simba, Pablo Franco ameweka wazi kuwa sababu kubwa ya timu hiyo kuachana na baadhi ya
mastaa akiwemo kiungo, Ibrahim Ajibu aliyejiunga na Azam ni kuwaambia wazi kuwa hawakuwa na nafasi ndani ya kikosi chake.
Simba ilitangaza rasmi juzi Alhamisi kusitisha mkataba na Ajibu kwa kile kilichoelezwa kuwa ni makubaliano ya pande zotembili, ambapo nyota huyo tayari ametangazwa kusaini mwaka mmoja ndani ya kikosi cha Azam.
Pamoja ana Ajibu, Simba kwenye dirisha hili la usajili inatarajia kuachana na nyota watatu wa kikosi hicho wakiwemo winga, Duncan Nyoni na kipa Jeremiah Kisubi ambao wanatarajiwa kutolewa kwa mkopo ili kuboresha kikosi chao na kusajili nyota wengine.
Akizungumza na Championi Jumamosi, kocha Pablo alisema: “Ni kweli tulifikia muafaka wa kuachana na baadhi ya wachezaji wa kikosi chetu na hii ni kutokana na ukweli kuwa nilikaa na wachezaji hao na kuwaweka wazi kuwa wasingekuwa na nafasi kwenye kikosi changu.
“Lakini pia baadhi yao walishindwa kufikia matarajio yao binafsi na ya klabu, hivyo kama wanadamu ni lazima pia tuangalie faida ya pande zote mbili na ndiyo sababu ya kuachana nao.”
Stori: Joel Thomas, Dar es Salaam