KOCHA Mkuu wa Simba, Pablo Franco ameweka wazi kuwa haridhishwi na namna ambavyo mastaa wa kikosi hicho wamekuwa wakishindwa kutumia faida ya mipira iliyokufa hususan penalti na tayari amekaa na mastaa hao ili kusaka suluhisho la changamoto hiyo.
Simba juzi Jumamosi waliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Azam katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa
kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam ambapo licha ya ushindi huo staa wao, Rally Bwalya alikosa mkwaju wa penalti.
Hii inakuwa ni penalti ya tatu kati ya nne ambayo Simba wamekosa katika michezo yao mfululizo ambapo Bwalya
amekosa penalti mbili, Morrison moja sawa na Erasto Nyoni.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Kocha Pablo alisema: “Tunashukuru kwa ushindi ambao tuliupata katika
mchezo wetu dhidi ya Azam, kwetu huu ulikuwa ushindi muhimu.
Lakini licha ya ushindi huo niweke wazi kuwa nimeshangazwa sana na namna ambavyo tumekuwa na wakati mgumu kutumia faida ya mipira iliyokufa hususan penalti.
“Ukiangalia vizuri utagundua kuwa tumekosa penalti tatu kati ya nne mfululizo kwenye michezo yetu iliyopita kupitia kwa wachezaji tofauti kama Morrison, Bwalya na Nyoni.
Ni kweli kukosa penalti ni sehemu ya mchezo lakini hii haitoi taswira nzuri kwangu kama kocha na tayari nimeanza kulifanyia kazi hilo.”
Stori: JOEL THOMAS, Dar es Salaam