Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini SACP David Misime, amesema Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi mkoani Mtwara Grayson Mahembe aliyejinyonga kwa dekio, alikuwa amewekwa kwenye mahabusu ya peke yake na wenzake walipelekwa kwenye mahabusu za Lindi ili wasiharibu ushahidi uliokuwa unakusanywa
SACP Misime, ametoa kauli hiyo hii leo Januari 31, 2022, wakati akitoa ufafanuzi wa Mkaguzi huyo aliyejinyonga Januari 22 mwaka huu baada ya kukutwa na tuhuma za mauaji ya kijana mkazi wa kijiji cha Ruponda wilayani Nachingwea mkoani Lindi aliyekuwa akiwadai askari 7 zaidi ya shilingi milioni 33.
"Mahembe alipohojiwa alieleza mtiririko mzima na kuwapeleka maafisa sehemu walipoutupa mwili wa Musa Hamis, aliwekwa katika mahabusu ya peke na ndivyo ilivyofanyika kwa wengine, baadaye alijinyonga taratibu zote zilifuatwa, alipigwa picha na zipo na zinaonesha dalili zote za mtu aliyejinyonga," amesema SACP Misime
Grayson Mahembe na wenzake saba, wanadaiwa kutekeleza mauaji ya kijana huyo Januari 5 mwaka huu na kisha mwili wa marehemu waliutupa katika kitongoji cha Majengo, kijiji cha Hiari wilayani Mtwara.