Dar es Salaam. Jeshi la polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limeeleza kuwa limewaua watu watatu wanaodaiwa kuwa majambazi waliokuwa katika mpango wa kupora katika duka moja la miamala ya fedha eneo la Mbagala Zakhiem.
Kwa mujibu wa Kamanda wa kanda hiyo, Jumanne Muliro tukio hilo lilitokea Januari 26, 2022 na wanaodaiwa kuwa watuhumiwa hao walikuwa wakitumia usafiri pikipiki aina ya Hoajue na baada ya kugundua kuwa wanafuatiliwa na polisi walianza kurusha risasi.
“Baada ya kuanza kurusha polisi walijihami kwa kutumia silaha ambapo waliwajeruhi na baada ya kufikishwa hospitali waligundua kuwa wameshapoteza maisha, uchunguzi wa kubaini mtandao wao bado unaendelea,” alisema Muliro.
Alisema baada ya ukaguzi walibaini kuwa marehemu walikuwa na bastola moja yenye risasi 11 na fedha bandia Sh1.18 milioni ambazo huzitumia kwa geresha kuwa wanataka kuweka fedha kisha kumvamia wakala kwa kumtolea bastola.
“Hiyo bastola ina uwezo wa kutunza risasi 25 ila tulikuta 11, maana yake 14 zilitumika na risasi 14 kwa maisha ya watu ni nyingi sana,” alisema Muliro wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisi za Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.
Alisema bastola waliyokuwa nayo ni muundo wa 75CAL 9 PARA, yenye namba K4596 iliyotengenezwa nchini Czechoslovakia.
Kamanda Muliro alisema si dhamira ya Jeshi la Polisi si kuwaua wahalifu, lakini nao hawako tayari kupoteza askari wao hata mmoja, hivyo ni lazima wajihami kwa mujibu wa sheria.