SILAHA ya jadi aina ya panga, ni moja ya vifaa vilivyokutwa katika shimo alilofukiwa mtu anayedhaniwa alikuwa muuguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya KCMC, Patricia Ibrock (66), anayedaiwa kuuawa na watu watatu akiwemo mwanae wa kumzaa mwaka jana.
Taarifa za awali kutoka Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro zimedai kuwa, binti huyo alishirikiana kufanya mauaji hayo akiwa na waganga wawili wa jadi kutoka Dar es Salaam na Tanga, huku mmoja wao akidaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na binti huyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa alisema jana kuwa, tukio la mauaji ya mama huyo lilitokea Februari, 2021 nyumbani kwake Kijiji cha Rau Mrukuti, Kata ya Uru Kusini, wilayani Moshi na kwamba jeshi hilo linawashikilia watu watatu akiwemo binti huyo.
“Wakati timu ya uchunguzi inafukua eneo lililofukiwa mwili wa mama huyo tulikuta mabaki ya mwili unaodhaniwa wa Patricia uliokuwa umefungwa na blanketi, vitu vya aina mbalimbali ikiwamo panga ambalo lilikuwa na mabaki ya nywele zinazodaiwa ni mama huyo,” alisema.
Hata hivyo, Kamanda Maigwa alisema majina ya watuhumiwa hao yamehifadhiwa kwani Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa kina ili kufahamu chanzo cha mauaji hayo na wahusika kutokana na mazingira ya tukio kuchukua takribani mwaka mmoja sasa.
Hata hivyo, Kamanda Maigwa alisema majina ya watuhumiwa hao yamehifadhiwa kwani Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa kina ili kufahamu chanzo cha mauaji hayo na wahusika kutokana na mazingira ya tukio kuchukua takribani mwaka mmoja sasa.
Alisema hofu ya kuwapo kwa mauaji hayo ilizuka baada ya binti huyo kuonekana akiwa na kasi isiyo ya kawaida ya kuuza mali za mama yake kwa madai ya kwenda kumfanyia matibabu nchini India lakini ndugu na jamaa hawakuwa wakimuona mama huyo hadharani.
“Uchunguzi unaonesha kwamba hadi mama huyo anauawa, tayari alikuwa ametumia Sh milioni 60 kwa ajili ya matibabu yaliyohusisha waganga hao bila kuwapo kwa matumaini ya kupona na baadaye inaonekana walikuwa wakishinikiza mama aongeze fedha nyingine ambapo alikaidi ndipo walimuua,” alisema.
Alisema fedha zilizokuwa zikitumika katika matibabu hayo ni mali ya mama huyo ambazo ni malipo ya fedha za kustaafu katika Hospitali ya KCMC.
Alisema baada ya mabishano na mama yake pamoja na waganga hao, watuhumiwa hao waliamua kumuua majira ya mchana kisha mwili kuuhifadhi ndani ya nyumba wakisubiri giza kuingia na baadaye wakachimba shimo dogo na kumfukia huku wakiwa wamemfunika kwa blangeti alilokuwa akililalia.
Kamanda Maigwa alisema mabaki ya mwili wa Patricia yanafanyiwa uchunguzi katika Hospitali ya KCMC, huku baadhi ya vifaa vilivyokutwa ikiwamo panga na vingine vinafanyiwa uchunguzi wa kina kisha upelelezi utakapokamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani.