MKOA wa Pwani nchini Tanzania, ‘umepiga bao’ mikoa mingine nchini humo kwa kutoa mawaziri na naibu mawaziri watano katiba Baraza la Mawaziri. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Katika baraza hilo la mawaziri 25 na naibu 26 lililotangazwa jana Jumamosi tarehe 8 Januari 2022 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Katanga, Pwani yenye majimbo tisa imeizidi mikoa mingine kama Dar es Salaam, Morogoro ambayo haina waziri wala mbunge.
Dar es Salaam yenye majimbo 10, ilikuwa na mawaziri wawili, Profesa Kitila Mkumbo wa Ubungo aliyekuwa waziri wa viwanda na biashara aliyewekwa kando kwenye mabadiliko haya pamoja na Dk. Faustine Ndugulile wa Kigamboni aliyekuwa waziri wa Teknoloajia ya Habari na Mawasiliano, aliyeachwa Septemba 2021.
Pia, Morogoro yenye majimbo 11 ilikuwa na waziri mmoja kutoka Kilosa, Profesa Palamagamba Kabudi wa Katiba na Sheria na baada ya kuenguliwa, sasa haina waziri ama naibu.
Kati yao, mawaziri ni wawili ambao ni Seleman Jafo, aliyeteuliwa kuendelea kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) anayetoka Jimbo la Kisarawe pamoja na Mohamed Mchengerwa, aliyeteuliwa kuwa waziri wa utamaduni, sanaa na michezo.
Waziri wa Muungano, Suleiman Jafo
Mchengerwa ambaye kitaalamu ni mwanasheria, anayetoka Jimbo ma Rufiji, amehamishwa wizara kutoka wizara ya utumishi na utawala bora ambako alikuwa waziri.
Naibu mawaziri walioteuliwa ni Abdallah Ulega wa Mkuranga kuendelea kuwa naibu waziri wa mifugo na uvuvi na Omary Kipanga wa Jimbo la Mafia, naye kuendelea kuwa naibu waziri wa elimu, sayansi na teknolojia.
Ingizo jipya kwenye baraza hilo kutoka Pwani ni Ridhiwani Kikwete, kuwa naibu waziri wa katiba na sheria.
Ridhiwani anayetoka Jimbo la Chalinze ni mtoto wa Rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete.