Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameruhusu Wafanyabiashara wa Soko la Karume kurejea na kuendelea na biashara kwa kuwekewa mpango mzuri ambapo Wafanyabiashara wa Soko hilo wamepongeza uamuzi huo na kuishukuru Serikali.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es aalaam, Amos Makalla ametangaza uamuzi huo leo wakati wa mkutano wake wa hadhara na Wafanyabiashara wa Soko la Karume baada ya kupokea taarifa ya ripoti iliyoundwa kuchunguza chanzo cha moto.
RC Makalla amesema Rais Samia ameelekeza pia uwepo utaratibu mzuri wa kuzuia moto, kuhakikisha hakuna atakayedhulumiwa eneo lake na kutoa ruhusa kwa Wafanyabiashara kujenga Vibanda kwa gharama zao.
Wafanyabiashara hao walizuiwa kwa muda wa siku saba kufanya biashara katika soko hilo ili kupisha uchunguzi wa chanzo cha soko kuungua ambapo RC Makalla amesema chanzo ni mshumaa wa Mateja.