RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewapongeza wenyeviti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kusimama kutetea mkopo wa Sh.1.3 trilioni. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Mkopo huo usiokuwa na riba ni kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) wenye lengo la kuchochea mapambano dhidi ya UVIKO-19.
Leo Jumanne, tarehe 4 Januari 2022, Rais Samia amepokea taarifa ya utekelezaji wa fedha hizo kwenye miradi mbalimbali ikiwemo ya elimu, afya, maji na miundombinu, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Amewapongeza viongozi mbalimbali wa Serikali na chama chake- Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kusimamia vyema fedha hizo na kuwajibu waliojitokeza kuhoji mikopo hiyo.
“Niwashukuru mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya kwa kusimamia miradi hii lakini niwashukuru zaidi na zaidi wenyeviti wa CCM kwa kusimama na kutetea mkopo huu ulioleta maendeleo. Walijotokeza kuhoji mkopo mlisimama na kusema,” amesema Rais Samia.
Viongozi hao wa CCM kama mikoa ya Mwanza, Kilimanjaro, Dar es Salaam, Singida na Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) walijotokeza kumjibu Spika wa Bunge, Job Ndugai.
Walimjibu baada ya Spika Ndugai kukosoa mkopo huo wa Sh.1.3 trilioni na kusema, bora kujibana kwa kutumia fedha za ndani kama tozo kugharamikia miradi ya maendeleo.
Spika Ndugai alikwenda mbele zaidi na kudai, iwapo madeni yatakuwa makubwa, yanawezekana nchi ikapigwa mnada.
Kauli hiyo ilimuibua Rais Samia na kusema serikali anayoingoza, itaendelea kukopa huku wenyeviti wa CCM wakimshambulia kama nyuki, Spika Ndugai wakimtaka kutomkwamisha Rais Samia.
Baada ya kushambuliwa vilivyo, jana Jumatatu tarehe 3 Januari 2022, Spika Ndugai alijitokeza kumwomba radhi Rais Samia na wananchi kwa kauli hiyo aliyoitoa.
Spika wa Bunge, Job Ndugai
Amesema, ameshangazwa na kiongozi huyo kusimama mbele za hadhara kukosoa mkopo huo wakati bajeti na taarifa mbalimbali zinapitia kwenye bunge lake, “na hiyo ni homa yam waka 2025.”
Rais Samia amesema, “nilipotishwa huu mzigo, kuna mtu alikuja akanipa pole na hongera na akasema atakayekusumbua kwenye kazi hii ni mwenye shati la kijani mwenzako si wa upinzani na hili ni wanaoitizama 2025.”
Akizungumza kwa sauti ya chini Rais Samia amesema, “kelele za wanaopiga kelele hawanisumbui ila na mimi nina moyo wangu si wa glasi ni wa nyama ulioumbwa na Mungu, nishikeni mkono twende sote.”