Rais Samia Suluhu Hassan
RAIS Samia Suluhu Hassan amesema baada ya ujenzi wa miundombinu ya elimu, kutoa vifaa vya kusomeshea, kujenga mazingira ya usomeshaji, ujenzi wa madarasa na kuwekea samani, kinachofuata sasa ni kuongeza ajira za walimu 6000 hadi 7000. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo tarehe 27 Januari, 2022 wakati akizungumza kwa njia ya simu na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Benjamini Mkapa iliyopo jijini Dar es salaam.
Wanafunzi hao na uongozi wa shule hiyo waliandaa sherehe kwa ajili ya siku ya kumbukizi ya Rais Samia.
Tuaongeza na kuwasambaza ili waendane na ujengaji wa madarasa na kiwango cha wanafunzi walioingia sekondari.
“Tunajua kwamba changamoto ipo kwenye shule za msingi, kwenye fedha za Uviko tumetumia vizuri kwenye shule shirikishi.
“Lakini kuna fedha ya tozo ambayo tunakusanya kila mwezi na tunaendelea kujenga madarasa katika ngazi ya msingi, katika ngazi hiyo bado kuna uhaba wa madarasa na furniture zake.
“Kwa hiyo kazi ndani ya sekta ya elimu ni kubwa nasi tutaendelea kuifanya kwa kushirikiana na wizara ya elimu lakini pamoja na Tamisemi wote kwa pamoja tukishirikiana,” amesema.
Aidha, katika hafla hiyo ambayo mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda kwa niaba ya Rais Samia, Kiongozi mkuu huyo wa nchi amewashukuru wanafunzi hao na wote walioandaa sherehe hiyo.
“Mwalimu mkuu wa shule, watumishi wote, shule na wanafunzi, pia shukrani ziende kwa ndugu yetu Mwijaku, Waziri wa elimu.
“Namshukuru pia Emanuel (mwanafunzi) mchumi wetu wa baadae, na wote waliochangia shughuli kuwa hivyo. Siku nzima wameitoa kwa ajili hiyo. Nawashukuru wote kwa moyo wa upendo,” amesema.
Aidha, ameahidi kushughulikia changamoto za shule hiyo zilizowasilishwa katika salama zilizotolewa na Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Deo Joseph.
“Mwalimu nimesikia changamoto ulizozisema, nimemsikia Waziri wa elimu amezibeba vizuri sana. Kwa hiyo vuta subira aniwasilishie mimi pamoja naye tutaamua ipi naibeba mimi kama rais. Ili tuondoshe hizo changamoto hapo shuleni.
“Lengo ni watoto wetu wapate kusoma vizuri zaidi na wawe na huduma nzuri zaidi. Nawashukuru naomba muendelee vema na shughuli yenu na Mungu awasimamie,” amesema.
Awali, Mwalimu Mkuu huyo akisoma salamu kwa mgeni rasmi, mbali na pongeza za siku ya kuzaliwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan amesema wanataka mwakani (2023) wawe ndani ya ukumbi wa mikutano kwa kuwa tayari michoro ipo na eneo la ujenzi lipo.
Ameomba chumba cha kupima uwezo wa kusikia ili kujua huduma gani zinahitaji kwa wale wanafunzi wenye changamoto ya kusikia.
“Pia tunaomba ikikupendeza utupatie gari la shule ambalo litasaidia kurahisisha huduma kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu kwa kuwa ni changamoto wakati wanapopata maradhi.
“Pia ikikupendeza tukawa na walau mabweni mawili ya wasichana na wavulana ili kupunguza usumbufu wanapohangaika na usafiri.
“Tunatanguliza shukra za dhati kwako Rais, umetenda makubwa umeifungua nchi, tunaamini mafanikio makubwa yanakuja,” amesems Mwalimu huyo.
Wakati Profesa Mkenda mbali na kuipongeza shule hiyo kwa kuendelea kupiga hatua katika ufaulu mzuri wa wanafunzi wa kidato cha nne, pia aliahidi kufikisha salama hizo kwa Rais Samia.