Rais Samia Atangaza Rasmi Uwepo wa Kirusi cha Omicron Tanzania

 


Ikiwa ni kawaida kwa kila awamu ya urais kuhutubia taifa ifikapo mwisho wa mwaka, Rais Samia Suluhu Hassan hii leo tarehe 31 Disemba amezungumza na wananchi kupiti vyombo vya habari.


Katika hotuba yake, Rais Samia amewakumbusha watanzania wote kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya UVIKO 19 kwa kuendelea kufuata ushauri wa wataalam wa afya na kupata chanjo ya ugonjwa huo akisisitiza kuwa kirusi kipya cha Omicron kinaenea kwa kasi na kimeshaingia nchini Tanzania.


“Dunia bado inakabiliwa na janga la UVIKO 19, na kwa sasa tupo katika wimbi la nne la ugonjwa huo. Kirusi kipya cha IMICRON kinaenea kwa kasi kubwa, na tayari kimeshaingia nchini kwetu,” amesema Rais Samia.


Aidha Rais Samia amewataka watanzania kujitokeza kwa wingi katika zoezi la sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 ili kuweza kupata takwimu zitakazosaidia kupanga kwa usahihi maswala yote ya maendeleo ya nchi.


“Mwaka 2022 ni mwaka wa sensa ya watu na makazi hivyo naendelea kuwahimiza watanzania kujitokeza kwa wingi kuhesabiwa.” Alisema Rais Samia


“Kwa watumishi wenzangu, niendelee kuwasihi watumishi wote wa umma na sekta binafsi tuingie mwaka wa 2022 kwa malengo ya kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.” Aliongeza


Rais Samia amesema mwaka 2022 ni mwaka wa kukabiliana na changamoto zinazopunguza uwezo wa wananchi katika kukabiliana na Maisha ya kila sikukwa kuwa mpango wa mwaka 2025/2026 wa serikali una lengo kuu la kukuza uchumi wa mtu mmoja na uchumi wa taifa.


Pamoja na mipango hiyo ya Serikali kwa mwaka 2022 Rais Samia pia amezungumzia vikwazo ambavyo nchi ilikutana navyo mwaka 2021 vilivyosababishwa na changamoto kubwa za UVIKO 19 zilizosababisha athari za kufungwa mipaka, mvua zilizozidi wastani zilizosababisha uharibifu wa miundombinu ya usafirishaji nchini na kuchelewesha utekelezaji wa miradi, mfumko wa bei ulifikia 4.1% uliosababishwa na kupanda kwa bei ya mafuta duniani na mfumko wa UVIKO 19.


“Kwa hapa nchini, mfumuko huo wa bei ulichagizwa zaidi na utekelezaji wa mpango wa maendeleo kwa ustawi wa taifa na mapambano dhidi ya UVIKO 19 uliotoa kiasi cha sh trilioni 1.3 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya afya, elimu, majisafi na salama, ambao ulisababisha upandaji wa bei za vifaa vya ujenzi kama saruji nondo na mabati,” amesema Rais Samia.


Rais Samia pia amezungumzia mafanikio ambayo watanzania waliyapata ikiwa ni pamoja na kuweza kudumisha amani na utulivu wa nchi, ukuaji chanya wa uchumi uliofanya nchi ya kuwa ya 19 kati ya nchi 54 za Afrika, hali iliyosababishwa na wananchi kuendelea na kazi zao za kiuchumi badala ya kuwafungia ndani kama nchi nyingine.


“Vile vile katika kuvutia uwekezaji na kurudisha fedha katika mzunguko, tulifanya marekebisho mbalimbali ya kisera kisheria na kikodi na kiutendaji. Matokeo yake tumeweza kuvutia uwekezaji kutoka miradi 186 yenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 113 mwaka 2020, hadi miradi 237 yenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 4141 mwaka 2021.” Aliongeza


Aidha Rais Samia alisema kuwa Pamoja na changamoto za UVIKO 19 bado serikali iliendelea na miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo ufuaji wa umeme Rufiji, upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam, ujenzi wa daraja la Kigomgo Busisi, ujenzi wa daraja la Tanzanite Dar es Salaam, upanuzi wa barabara za viwanja vya ndege, barabara kadhaa zinazounganisha mikoa na wilaya nchini na kuendeleza ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR.


Aidha Rais Samia ametoa rai kwa kikosi kazi kilichoundwa na msajili wa vyama vya siasa kufanyia kazi kwa weledi maazimio ya mkutano wa vyama vya siasa na serikali itapokea mapendekezo yatakayotolewa na kuchukua hatua stahiki ili kuhakikisha kunakuwa na mazingira mazuri ya kisiasa.


Katika kukamilisha hotuba yake, Rais Samia amewatakia wananchi wote heri ya mwaka mpya na kuwasihi kuwa makini barabarani, na kuwaandaa watoto kuendelea kunufaika na fursa adhimu ya elimu bila malipo.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad