Dar es Salaam. Mshumaa uliowashwa na ‘mateja’ waliokuwepo katika Soko la Karume ndio chanzo cha moto mkubwa uliotokea usiku wa kuamkia Januari 16, 2022 na kusababisha hasara ya Sh7.2 bilioni, kwa mujibu wa ripoti ya uchunguzi.
Akikabidhi ripoti hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla na viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama, Mwenyekiti wa kamati ya uchunguzi, Justine Lukaza amesema mateja hao walikuwa wanavuta dawa za kulevya katika moja ya kibanda katika soko hilo.
Amesema uchunguzi umebaini kuwa vijana wapatao watano (majina wanayo) ambao walitumia mshumaa kumulika kwa ajili ya mwanga ndio waliosababisha janga hilo.
"Kijana mmoja wao tuliyemhoji kwa sura anaonekana ni mrahibu wa dawa za kulevya na alikiri walitumia, kisha wakasinzia. Na mashuhuda wanasema kama sio kuwahi kuwatoa basi tungesema mengine.
"Lakini pia tuliangalia sababu za moto kusambaa kwa haraka ni aina ya vifaa vya ujenzi, ambapo vibanda vimejengwa kwa kutumia mbao na milunda. Moto ulianza saa 7 usiku na taarifa zinaonesha aliyepiga simu alipiga saa 9:11usiku, lakini askari doria baada ya kuona moto unaendelea alienda moja kwa moja kuripoti zimamoto saa 8:33 usiku. Gari la zimamoto lilifika pale saa 9:14. Hiyo pia ilichangia pamoja na miundombinu ya kufika ilisababisha moto kuwaka kwa haraka sana," amesema.
Akiwasilisha maoni na mapendekezo, Katibu wa Kamati hiyo, Omary Dosho amesema kwa kuwa eneo hilo ni mali ya serikali inashauriwa lijengwe na Serikali kisha vizimba vigawiwe upya kwa wafanyabiashara kwa mikataba maalumu.
Amesema wamependekeza Serikali itafute fedha ili soko lianze kujengwa kwa haraka na Halmashauri iweke usimamizi madhubuti kwa vigezo vya wafanyabiashara kuitwa wamachinga.
"Na hii ni kwa sababu tumebaini wafanyabiashara wanaofanya katika soko hilo mitaji yao imekuwa, wapo ambao wanamitaji hadi milioni 50 kiasi kinachokinzana na sheria ya kodi," amesema.