Sabaya Aeleza Jinsi Alivyotegwa Kwa Kutumia Wafanya Biashara Wenye Ushawishi




Arusha. Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya amesema aliyekuwa Mbunge wa Hai na mwenyekiti wa chama cha upinzani Taifa (ambaye hakumtaja jina), aliwatumia wafanyabiashara wenye ushawishi kuhakikisha anaingia matatizoni.

Sabaya ametoa madai hayo jana, mbele ya Hakimu Mkazi Patricia Kisinda wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha wakati akiulizwa maswali na wakili wa utetezi, Sylvester Kahunduka.

Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi, Sabaya anashtakiwa pamoja na Enock Mnkeni, Watson Mwahomange, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya. Sehemu ya mahojiano hayo ilikuwa kama ifuatavyo:

Wakili: Kuna wakati ulilalamika kuwa shahidi wa 13 wa Jamhuri anashirikiana na watu kukuangamiza uonekane una ‘image’ mbaya kwa jamii, ulikuwa unamaanisha kitu gani?


Shahidi: Mimi nilikuwa mkuu wa Wilaya ya Hai, ni jimbo la uchaguzi ambapo kulikuwa na mbunge ambaye aliamini hawezi kuacha ubunge maisha yake yote. Mbunge huyo ambaye ni mwenyekiti wa chama cha upinzani Taifa alitumia ushawishi wake akidhani mimi ndiyo nazuia ubunge wake wa mwaka 2020, alitumia ushawishi wake wote kuhakikisha ananidhibiti ili apate ubunge na aliwatumia wafanyabiashara ili niingie kwenye matatizo na amefanikiwa.

Soma zaidi: Magufuli atajwa tena kesi ya Sabaya

Mheshimiwa hakimu kuwa mbele yako leo nikiwa hai nashukuru, kwani mipango iliyokuwepo ni ya kuondoa kabisa uhai wangu. Katika siasa hizo sikutegemea shahidi wa 13 angeingia kwenye mtego wa kufanya siasa katika mazingira ambayo mimi tu nilipewa haki ya kusikilizwa na nilinyimwa kwa makusudi.

Wakili: Umesema alichoelekeza Rais sicho kilichofanyika, ulikuwa unamaanisha kitu gani?

Shahidi: Rais alitoa maelekezo ya kunisimamisha ili kupisha uchunguzi na ilikuwa busara, unachunguza jambo ambalo huna uhakika nalo, ndiyo maana nilipaswa kupewa haki ya kusikilizwa na sikuwahi kupewa hiyo haki.

Awali, wakili wa utetezi, Fridolin Bwemelo anayewatetea washitakiwa wa tatu na nne, alimhoji Sabaya pia, lakini Wakili wa Serikali Mwandamizi, Janeth Sekule aliiomba mahakama kuahirisha kesi hiyo hadi Jumatatu itakapoendelea na hakimu alikubaliana na ombi hilo na kuiahirisha kesi hiyo hadi Februari 2 upande wa Jamhuri utakapoanza kumuuliza maswali ya dodoso
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad