RAIS Samia Suluhu, ambaye leo anatimiza miaka 62 amesema alianza kusaka ajira akiwa na umri mdogo ambapo awali alikataliwa kutokana na sheria ya ajira kwa watoto.
Anasema iyo ilikuwa ni mwaka 1977 akiwa na umri wa miaka 17 ambapo alilazimika kukaa nyumbnai kwa miezi sita ndio baadae akaitwa kuanza kazi idara ya masijala.
“Niliajiriwa nikiwa mdogo sana mwaka 1977 nikiwa na wa miaka 17 hivi na nakumbuka nilipokwenda kwenye ajira mara ya kwanza wakasema nenda nyumbani, hapa tutafanya child labor kwa hiyo rudi nyumbani, nikarudi nyumbani nikakaa nyumbani miezi sita hivi halafu ndio wakaniita tena” anasema Rais Samia katika mahojiano maalumu na Jambo Tanzania ya TBC.
Anasema ingawa alipata kazi hiyo lakini aliona kuwa nafasi hiyo lakini aliona kabisa pale si pake na kuamua kuongeza elimu.
“Niliajiriwa mwaka 1977 nikiwa karani masijala lakini nilikuwa najiona kabisa pale sio mahala pangu, kwa sababu nilikuwa nafanya kazi zaidi kuliko waliokuwa wanashika madeski, nilifanya kazi sawasawa na maofisa, na ndicho kilichonifanya niondoke nikaongeze elimu na baada ya kuongeza elimu nikaajiriwa na Shirika la Chakula Duniani, nikafanya kwa miaka tisa, nikarudi tena serikalini,” amesema.
Ameongeza “Nikarudi serikali kwa sababu nilishazoea kuchakarika huko kwenye mashirika, serikali niliona kama nabanwa, mnajua serikali ni kama mikono imefungwa, unabanwa, nikaona hapana, nikaondoka nikaenda kufanya kazi kwenye NGOS ya Angoza nikikaimu nafasi ya Ukurugenzi na baadae kuwa Mkurugenzi.