Mwenyekiti wa mtaa wa Dome Akizungumza na wazazi.
Shinyanga. Baadhi ya wazazi wa mtaa wa Dome Kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga wameiomba Serikali ikae na kutathimini upya suala la watoto wa kike kuendelea na masoma katika mfumo rasmi baada ya kujifungua.
Ombi hilo wamelitoa jana Januari 10, kwenye kikao cha mtaa huo, ambapo wazazi na walezi wenye watoto waliofaulu kuingia kidato cha kwanza wameaswa kutovunjika moyo kuwasomesha watoto wao.
Novemba 2021, aliyekuwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alitangaza rasmi kuwaruhusu wanafunzi waliokatiza masomo yao kwa kwasababu ya kupata ujauzito wakiwa shuleni kurejea masomoni kupitia mfumo rasmi.
Wakizungumza katika kikao hicho, baadhi ya wazazi akiwamo Said Yusuph na Yunis Charles wamesema, endapo wasichana wataendelea na shule, huku wakiwa wananyonyesha watasababisha watoto wengine waone kuwa ni kitu cha kawaida kwenda shuleni huku wakiwa na watoto.
Naye Suzana Nkandi ambaye ni mkazi wa mtaa huo amesema watoto wa kike waliojifungua hawatakiwi kuchangamana na watoto wa kike ambao hawajajifungua kwani wakichangamana shule moja watawapotosha na wenzao ambao hawajawahi kuzaa na hawatasoma vizuri wataendelea kuwaza watoto wao tu, labda wajengewe shule yao wawekewe na walimu.
"Mimi binafisi sikubaliani kabisa na suala hili la Serikali. Nimesikia fomu za kujiunga watoto hawa zipo hapa kwa mwenyekiti, lakini sijaafiki hata kidogo msichana mwenye mtoto arudi shuleni, kwani anaporudi shuleni anamuachia nani mtoto wake?
“Inamaana bibi wa mtoto huyo atafute hela za daftari huku akiwa amebeba mjukuu mgongoni," amehoji Adrofina Sprian.
Hoja hiyo imeungwa mkono na Yunus Charles akisema; "Sisi wazazi wa wasichana tunahangaikia watoto wale, halafu tena mtoto wangu wa kike aliyefanya ujinga wake akapata mtoto aniachie mtoto wake nitafute chakula nikiwa na mjukuu mgongoni nitaweza kweli?
“Hilo kwa kweli haliwezekani wapambane wenyewe na watoto wao hatuko tayari kabisa kulea watoto maisha yenyewe ni magumu mno."
Kwa upande wake Ofisa Elimu kata ya Ndembezi, Ustadius Mkulu amesema, Serikali haijawalazimisha wazazi kuwapeleka shule watoto wa kike waliojifungua, bali wakiona kuna umuhimu wa kuwaendeleza watafanya hivyo.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Dome, Solomon Najulwa amesema; “Kila mmoja aangalie faida ya kumpeleka shule mtoto wake. Serikali haijawalazimisha wazazi. Wakaokubali watatengewa madarasa yao binafsi ili waweze kupata elimu na watimize ndoto zao.
“Kna shuhuda nyingi za waliopata ujauzito kwa vishawishi walisoma na walifanikiwa, wengine walibakwa, hivyo wasichana kama hao ukiwaendeleza wanaweza kufika mbali na mzazi akashangaa,” amesema.