SHIRIKA la Afya Duniani Limedai Virusi Vipya vya Corona, Omicron, Vimeishiwa nguvu barani Afrika


SHIRIKA la Afya Duniani (WHO) limesema kuwa aina mpya ya virusi vya corona, Omicron, imeishiwa nguvu barani Afrika.

Mkurugenzi wa WHO anayehusika na hali ya dharura ya kiafya barani Afrika, Abdou Salam Gueye, jana Ijumaa alisema kuwa Afrika inaelekea kujinasua na wimbi la nne la maambukizi ya corona yaliyochochewa na Omicron.

Afisa huyo alisema maambukizi yamekuwa yakipanda kwa kasi kwa wiki sita mfululizo lakini sasa kasi hiyo imeshuka.

Wimbi la Omicron, kulingana na mkurugenzi huyo, ndilo lililodumu kwa muda mfupi zaidi barani Afrika.


Gueye alielezea wasiwasi wake kuhusu idadi ndogo ya watu ambao wamepokea chanjo ya corona barani Afrika.

WHO, hata hivyo, maambukizi ya Omicron katika yangali juu nje ya bara la Afrika.

Wiki iliyopita, shirika hilo lilisema kuwa zaidi ya watu milioni 15 waliambukizwa virusi vya Omicron ndani ya siku saba.


Shirika la WHO linatabiri kuwa asilimia 60 ya watu duniani wataambukizwa virusi vya Omicron kufikia Machi 2022.

Nusu ya watu barani Ulaya wanatarajiwa kuambukizwa virusi vya Omicron kufikia mwishoni mwa mwezi ujao wa Februari, kulingana na WHO.

Wakati huo huo, Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (Unicef) limeelezea wasiwasi wake kuhusu mamilioni ya dozi za chanjo ya corona zinazoharibika kabla ya kutumiwa barani Afrika.

Kwa mujibu wa Unicef, idadi kubwa ya dozi zinazoharibika ni zili ambazo zimekuwa zikitolewa kama msaada kwa mataifa ya Afrika huku zikiwa zimesalia na muda mfupi kabla ya kuharibika.


Katika taarifa yake kwa Bunge la Ulaya, Unicef ilisema nchi tajiri zinazigawia nchi masikini chanjo ambazo muda wake wa mwisho kwa matumizi salama unakaribia.

Shirika hilo lilisema lilisema kuwa nchi nyingi za Afrika hazina vifaa vya kuhifadhi chanjo hizo hivyo kuzifanya kuharibika.

Serikali ya Uganda jana Ijumaa ilisema kuwa inatarajia kuharibu dozi 400,000 za chanjo ya corona ambayo imeharibika.

Waziri wa Afya Jane Ruth Aceng, alisema kuwa chanjo hiyo ilipelekwa kaskazini mwa nchi hiyo lakini haikutumika.


Nyingi ya chanjo zilizoharibika ni Moderna na AstraZeneca, kulingana na Aceng.Alisema wakazi wa maeneo ya Teso na Lango wamekataa chanjo hivyo kuisababisha kuharibika.

Hayo yanajiri huku Taasisi ya Kudhibiti Magonjwa (CDC) – Africa, ikisema kuwa inafanya juhudi kupata dawa ya Paxlovid, ambayo imeonyesha ufanisi wa asilimia 90 kumaliza makali ya corona na kuzuia waathiriwa wa maradhi hayo kulazwa hospitalini.

Mkuu wa CDC- Africa John Nkengasong alisema wanafanya mazungumzo na kampuni ya kutengeneza dawa ya Pfizer ambayo inamiliki dawa ya tembe ya Paxlovid, ili kuweza kuiagiza kwa ajili ya nchi za Afrika.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad