Shisha Kirusi Kipya Hatari kwa Mastaa...Baada ya Makonda Kuondoka Wanavuta Bila Woga

 

PAMOJA na kupigwa marufuku nchini Tanzania, lakini kasi ya uvutaji wa kilevi aina ya shisha, imerejea upya na kusababisha hatari kwa baadhi ya mastaa Bongo, ripoti ya Gazeti la IJUMAA inatisha.

UVUTAJI SHISHA WAREJEA KWA KASI

Uchunguzi wa Gazeti la IJUMAA umebaini kwamba, kilevi hicho ambacho ni kirusi kipya kwa baadhi ya mastaa Bongo, kimerejea kwa kasi ya ajabu kwenye sehemu mbalimbali za burudani na starehe jijini Dar na kinatumika hadharani kabisa, tofauti na miaka kadhaa iliyopita.

Wapo baadhi ya mastaa na watu wa kawaida ambao tayari wameonja madhara yake ikiwemo kuzimika na kuibiwa vitu mbalimbali.

Uchunguzi wetu umebaini kwamba, ongezeko la watumiaji wa shisha jijini Dar na baadhi ya miji mikubwa nchini Tanzania limesababisha madhara makubwa kwa jamii na hata kuhatarisha afya zao.

Hii ni kutokana na baadhi ya watumiaji kutumia kifaa kimoja kinachokuwa kimechanganywa tumbaku na dawa nyingine haramu za kulewesha kwa muda mfupi.

Baadhi ya watu wanadai kwamba, shisha imeongeza matumizi ya dawa za kulevya kwa sababu wengine wanachanganya kwenye kilevi hicho.

WOLPER, TUNDA WAPATA MADHARA


Miongoni mwa mastaa ambao wamepata madhara ya shisha ni pamoja na mwanamama mwigizaji wa Bongo Movies, Jacqueline Wolper, Tunda na wengine wakidai kuwekewa madawa ya kulevya na wengine sumu za kuwalewesha.

Kwa mujibu wa mwanamama Tunda ambaye ni video vixen maarufu Bongo, alijikuta akizima kwa siku nzima baada ya kutumia kilevi hicho aina ya shisha kinachopatikana jijini Dar ambapo alikuwa na haya ya kusema; “Shisha za Dar acheni ubabaifu, unamuwekeaje mteja vitu vya ajabu kwenye shisha anazima siku nzima, unafaidika nini, ni ushamba, hata siyo ujanja na tunazi-report sehemu zenye ubabaifu wa dizaini hizo iwe fundisho kwa wengine.”

YUMO PIA UWOYA

Baadhi ya mastaa ambao wamekwishajionesha hadharani hivi karibuni wakivuta shisha ni pamoja na mwanamama mwingine mwigizaji wa Bongo Movies, Irene Uwoya na warembo wengine wasiokuwa na majina makubwa kwenye sanaa.

Baadhi yao wamekuwa wakidai kwamba, zile wanazovuta wao hazina madhara kwa kuwa kilevi chake ni kidogo mno na wanachofurahia ni ladha yake ya vanilla, strawberry, mint, chocolate au kahawa, bila kujua madhara ya kilevi hicho ambayo yanatajwa kuwa ni makubwa.

MAMLAKA YAPIGA MARUFUKU

Hata hivyo, tayari Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) iliyo chini ya Kamishna Jenerali Gerald Musabila Kusaya imepiga marufuku matumizi ya kilevi hicho nchini Tanzania

Katika ufafanuzi wake, Kamishina Msaidizi wa Kinga na Huduma kwa Jamii wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA), Moza Makumbuli anasema kuwa, kitendo cha mtu kuvuta shisha kwa saa moja ni sawa na mtu kuvuta sigara kati ya 100 hadi 200, jambo ambalo ni hatari zaidi kiafya.

Anasema kuwa, hali hiyo imekuwa ikichochewa na watu wenye nia mbaya ambao huwa wanaongeza madawa ya kulevya katika mchanganyiko huo ili kupata kilevi.

Anaendelea kusema kuwa, uhalifu wa dawa za kulevya upo mitaani na kila mmoja atambue kuwa, shisha ni utamaduni ambao umekuja nchini kutoka nje na haupaswi kupewa nafasi katika jamii zetu.

Katika kuhakikisha, mamlaka hiyo inachukua hatua za haraka kudhibiti matumizi ya shisha na aina nyingine za dawa za kulevya, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kuzuia Dawa za Kulevya, Florence Khambi anasema kuwa, mamlaka inafanyia kazi na taarifa zaidi na itakuwa inazitoa ili kuhakikisha Taifa linakuwa salama bila dawa za kulevya.

MADHARA YA SHISHA

Kamishna Msaidizi Makumbuli anasema kuwa, kwa sasa tatizo kubwa linaloikumba jamii ni kukithiri kwa matumizi ya dawa zilizochepushwa kutoka katika matumizi halali na kugeuzwa dawa za kulevya.

Anasema kuwa, watumiaji wa shisha wanapaswa kutambua kuwa ina madhara mengi na hatari kwa afya ya binadamu.

SHISHA NI NINI?

Kwa mujibu wa wauzaji waliozungumza na Gazeti la IJUMAA kwenye maeneo ya starehe hasa kwenye Ufukwe wa Bahari ya Hindi jijini Dar, shisha ni tumbaku iliyochanganywa na ladha za harufu za kuvutia kama matunda aina mbalimbali ikiwemo vannila au chocolate.

Wanasema kuwa, shisha inavutwa tofauti kidogo na sigara; yaani inavutwa mara nyingi kwa muda mfupi, huvutwa ndani zaidi ya mapafu na kwa kutumika muda mrefu; yaani zaidi ya saa moja tofauti na sigara ambayo inavutwa dakika tano na kuisha.

Kwa mujibu wa wataalam, tofauti na sigara ambayo inasababisha saratani ya mapafu tu, mara nyingi shisha inaleta saratani mbalimbali ikiwemo za figo, koo, mapafu, kibofu cha mkojo, ubongo na damu kwa wakati mmoja.

Pia wanasema kuwa, matumizi ya shisha huwa yanasababisha kusambaza magonjwa kwani mara nyingi shisha inatumika na watu zaidiya mmoja, wakati mwingine hata wasiofahamiana. 

Wanahitimisha kwa kusema kuwa, shisha ni kirusi hatari kiafya kwani huwa inachangia kwa kiwango kikubwa magonjwa ya kinywa na kansa ya koo.

KAMA UMEATHIRIKA, UFANYE NINI ILI KUJINASUA?

Kamishina Msaidizi Makumbuli anasema kuwa, kuna namna nyingi ambazo mtu anaweza kujinasua katika matumizi ya shisha na dawa za kulevya kwa jumla.

“Mosi ni kujitambua kuepuka makundi hatarishi, kuepuka tamaa, kutoa taarifa kwa wakati kuhusiana na watu au kikundi cha watu ambacho kinajihusisha na biashara ya dawa za kulevya ikiwemo kuepuka unyanyapaa kwa waraibu wa dawa za kulevya, badala yake kuwa nao karibu na kuwapa elimu kuhusiana na athari za matumizi hayo,” anasema.


GPL

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad