Dar es Salaam. Ajali ya kutisha imetokea Kimara Suka mkoani Dar es Salaam ikihusisha lori ambapo baadhi ya watu wanahofiwa kupoteza maisha huku wengine wakijeruhiwa katika ajali hiyo.
Mashuhuda wa ajali hiyo wameeleza kwamba ilitokea saa 12:15 alfajiri katika kituo cha daladala ambacho kipo jirani na alama ya kivuko cha wenda kwa miguu (Zebra).
Shuhuda wa ajali hiyo, Sikujua Mwaisaka ambaye anakatisha tiketi za mabasi yaendayo haraka (Dart) katika kituo hicho, amesema alianza kusikia vilio vya watu "nakufa, nakufa" na ghafla lori hilo likasimama mbele ya ofisi yake.
"Kuna wanafunzi walikuwa wanataka kuvuka barabara hapa, lori likatoka huko likawagonga wote, nilikuwa nasikia vilio tu huku wengine wakiwa wamelala.
"Nimeshuhudia miili ya watu saba kwenye uvungu wa lori, sijui kama huko nyuma kulikuwa na wengine. Wengine waliangulia pembeni wakiomba msaada," amesema shuhuda huyo.
Amesema walipiga simu polisi, wakafika kuchukua miili ya watu wanaodhaniwa wamepoteza maisha pamoja na majeruhi wengine waliokiwepo kituoni hapo.
Amesema baada ya muda, dereva wa lori alifika na kudai kwamba lori hilo lilichukuliwa na kondakta wake akiwa amelala bila kumpa taarifa.
Shuhuda mwingine, Damian Lusaka amesema ajali hiyo imehusisha pia bajaji ambayo ilikuwa na watu ndani yake baada ya kugongwa na lori hilo.
"Unajua hiki kituo kinatumiwa na watu wa bajaji pia, kulikuwa na bajaji hapa imepakia abiria, ikagongwa pamoja na watu wengine waliokuwepo hapa kituoni," amesema.
Majira ya 2 asubuhi, Mwananchi ilifika eneo la tukio na kushuhudia lori likiwa pembeni ya barabara huku damu zilizotapakaa barabarani zikifukiwa kwa mchanga. Baadaye lori hilo liliondolewa ili kuruhusu watumiaji wa barabara kuendelea na shughuli zao.
Hata hivyo, wakazi wa eneo hilo wanadai kwamba eneo hilo limekuwa na ajali nyingi ambazo zimekuwa zikichukia maisha ya watu, wanataka kituo hicho kihamishwe na pia wajengewe daraja litakaloungana na alama ya Zebra.
"Mimi hapa nimeshuhudia ajali zaidi ya tano, hapa hapa tu. Tunaomba hiki kituo kihamishwe kwa sababu kinatumiwa na mabasi ya mwendokasi, mabasi ya kawaida, bajaji pamoja na watu wanaokuja kupanda daladala. Sasa hapo kuna usalama?" amehoji Zuwena Khalid, mkazi wa Kimara Suka.