Simba ina Sapraizi yenu, Barbara Afunguka



MASHABIKI wa Yanga wamekuwa wakitamba sana mitaani na mitandaoni, kwamba msimu huu chama lao,ndilo litakalobeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara, lakini mabosi wa Simba wamejibu kimtindo kwa kuwaambia; ‘Tumewasikia, ila mjiandae kwa sapraizi bab’kubwa’.

Simba ndio mabingwa wa Ligi Kuu Bara kwa misimu minne mfululizo na sasa ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 24 kwa kucheza mechi 10, nyuma ya Yanga inayoongoza msimamo kwa pointi 29 zilizotokana na michezo 11 iliyocheza.

Licha ya Yanga kuwa kinara na kuonekana kuwa moto, mabosi wa Simba wakiongozwa na Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez amewatuliza wanachama wa klabu hiyo, kuwa watulie kwa vile wapo kazini kuhakikisha timu yao inarejea na moto kwenye mechi za Ligi Kuu.

Barbara alisema ni kawaida kwa mechi za mwanzoni mwa misimu karibu minne sasa, Simba kuwapata ugumu kutokana na kukamiwa na timu pinzani, lakini kadri siku zikisonga mambo yanakuwa mazuri.


Barbara alisema, kama viongozi na wakishirikiana na benchi la ufundi la timu hiyo chini ya Pablo Franco wamejipanga kuhakikisha wanarudi kwenye ligi wakiwa na moto, lakini wakitimiza pia malengo yao kwa msimu huu katika michuano ya kimataifa.

Simba ni wawakilishi pekee wa Tanzania kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho ikipangwa Kundi D sambamba na Asec Mimosas ya Ivory Coast, US Gendarmarie ya Niger na RS Berkane ya Morocco na itaanza mechi yao ya kwanza nyumbani dhidi ya Asec, Februari 13.

Timu hiyo iliangukia kwenye michuano hiyo baada ya kung’olewa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Jwaneng Galaxy ya Botswana iliyotoka nayo sare ya mabao 3-3 katika mechi zao mbili na Waswana kufuzu kwa faida ya bao la ugenini.


“Wanasimba wasiwe na hofu, viongozi wao pamoja na makocha wetu tupo makini na tutawasapraizi watu katika msimu huu, kama tunavyofanya misimu mingine yote ya nyuma. Hata hizi kelele za usajili wanachama wetu hawapaswi kuwa na presha,” alisema Barbara.

Msimu uliopita Yanga iliongoza msimamo kwa muda mrefu kabla ya Simba kutetea taji kwa mara ya nne kwa kukusanya pointi 83 dhidi ya 74 za Yanga zote zikicheza mechi 34.

Barbara alisema, wamegundua katika mechi zao za awali inazocheza timu yao wachezaji wa timu pinzani wamekuwa wakicheza kwa nguvu na kukamia kwa nia ya kusaka nafasi za usajili ndani ya kikosi chao na timu nyingine na sasa wameshatafuta dawa ya kuibeba timu yao.

Kuhusu usajili, alisema kwa sasa wamekuwa wakipata maombi mengi ya wachezaji kutoka nje ya nchi kupitia makocha, wachezaji na mawakala wao ndio maana baadhi wamewaita ili waonwe na kocha wao, kisha kuamua kama wawachukue au la kwa watakachokionyesha.


“Kikosi chetu kina wachezaji wengi wazuri jambo la kwanza kuna tuliowaacha ili ipatikane nafasi ya kuingiza wapya kutokana na mapendekezo ya kocha Pablo Franco,” alisema Barbara na kuongeza;

“Hivyo kutokana na mkakati wetu tuliokuwa nao viongozi kwa kushirikiana na Pablo tunahitaji wachezaji walio kwenye kiwango bora na kuisaidia timu wakati huu. Niwatoe hofu katika usajili wa wakati huu tutasajili kabla dirisha halijafungwa.

“Tutafanya hivyo ili kuhakikisha tunasuka kikosi imara ambacho Pablo hatapata wakati mgumu kufanya kazi na kufikia malengo ya kuchukua mataji mbalimbali tuliyokubaliana.”

Barbara aliwataka wanachama na mashabiki wao watulie kwani wana sapraizi kabla dirisha halijafungwa.


Licha ya Barbara kutofunguka sana, lakini Mwanaspoti linafahamu tayari kuna mazungumzo yanayoendelea kwa baadhi ya wachezaji waliopo nchini ili kuimarisha kikosi na kuziba nafasi zilizoachwa.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad