Simba Inakwama Hapa..Pablo Magulu Waibuka na yao..Edo Kumwembe Amtaja Chama




KOCHA wa Simba, Pablo Franco ameonyeshwa mambo yanayoweza kuichomoa Simba katika kipindi hiki cha mpito na kurejesha ubora wake kwenye Ligi Kuu Bara inayoendelea.
Uchovu wa wachezaji wa wa kikosi hicho, Ubora wa Yanga msimu huu, ushindani wa ligi na ukosefu wa mbinu mbadala haswa kwenye viwanja chakavu ni kati ya sababu kubwa zilizotajwa na wadau wa soka kuwa ndio chanzo cha kiwango kisichoridhisha cha mabingwa hao watetezi. Kocha mzoefu, Hababuu Ally amesema: “Inafikirisha sana, washambuliaji watatu katika mchezo mmoja wakose nafasi ya kufunga na wakati hao hao ndio walikuwa vinara msimu uliopita, ubutu wa washambuliaji wao unawagharimu sana.”

Alisema kuwa Pablo anatakiwa kuijenga timu ili mchezaji anayetoka na anayeingia wawe bora katika kila mchezo na sio akiumia mmoja timu inahaha.

Hababuu alisema Simba ya sasa imekuwa na mipango mingi midomoni kuliko ndani ya uwanja jambo ambalo ni shida kubwa.

Edo Kumwembe ambaye ni mmoja wa wachambuzi alisema Simba ni ileile,ili waweze kurejea kwenye mstari, wanapaswa watulie na kupambania pointi zilizopo mbele yao. “Sijaona tatizo kwenye kikosi cha Simba,kimetoka kutinga hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika,imechukua taji la Mapinduzi kwa mafanikio hayo unaanzaje kusema Simba ni mbaya,”alisema Kumwembe na akaongeza kuwa;

“Ndani ya kikosi chao, wamemuongeza Clatous Chama ambaye naamini atakuwa na mchango mkubwa, lakini pia wajue namna ya kukabiliana wapinzani wao kwenye viwanja vigumu,”alisema.

Beki wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa alisema hajaona shida ya timu hiyo; “Ikumbukwe kwamba kikosi cha Simba ambacho kimenyakua mataji ya ligi kuu mara nne mfululizo na kufanya vizuri Caf ni kilekile ndio maana nasema sijaona ubaya wake zaidi ya uchovu, labda kocha aanze kuwapa nafasi wale ambao walikuwa hawatumiki sana, huku wengine wakipumzika.”

PABLO, MUGALU WAFUNGUKA

Kocha wa Simba, Pablo Franco amekiri kuwa kuna programu maalumu ya kufanya mazoezi mengi aina mbalimbali ya kufunga katika uwanja wa mazoezi ili kila mchezaji anayecheza eneo hilo kufunga mabao mengi kuanzia sasa.

Alisema aina hiyo ya mazoezi ya kufunga itatengeneza hali ya kujiamini kwa wachezaji wake.

“Ukiangalia kikosi chetu kinatengeneza nafasi nyingi za kufunga mabao katika kila mechi ila kuna shida kidogo kama ya kukosa utulivu kwenye mashambulizi hayo,” alisema Pablo na kuongeza:

“Yote hayo tumefanyia kazi katika uwanja wa mazoezi, tutafanya vizuri kwenye mechi zijazo.”

Naye Mugalu alisema ni upepo mbaya tu unaopita ambao wamekutana nao lakini jambo hilo linachangiwa pia na kutoka katika majeraha yaliyokuwa yakimsumbua.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad