Somo: Usiahidi Chochote Kwa Mtu Mwenye Uhitaji, ikiwa Huna Hakika ya Kutimiza Ahadi yako




Ilikuwa ni wakati wa baridi kali. Barafu zilianguka toka mawinguni na kuenea kila kona ya mji. Jua halikupata kuchomoza kwa takribani miezi mitatu mutawalia.

Siku moja, tajiri mmoja akiwa akiwa nyumbani kwake, alimwona ajuza akipita nje ya nyumba yake akiwa amejikunyata—huku akitetemeka—kwa baridi. Nguo zake nyepesi na chakavu zilionesha kila dalili ya kushindwa kudhibiti wala kuhimili baridi ile.

Hii haikuwa mara ya kwanza kwa tajiri huyu kumwona Ajuza yule akipita nje akiwa katika hali ile. Akashindwa kuvumilia. Akatoka nje na kumwita.

Ajuza alipofika, tajiri akamwuliza: "Bibi inakuaje kila siku unatembea kwenye baridi kali namna hii bila ya koti wala shuka?"

Ajuza akajibu: "Sina koti wala shuka. Nguo pekee nilizonazo ni hizi nilizovaa. Kila siku inanilazimu kutoka ili kujitafutia riziki."

Tajiri akasema: "Nisubiri niingie ndani kukuangalizia makoti pamoja na shuka."

Ajuza alibaki nje akimsubiri tajiri kwa furaha na faraja kubwa.

Tajiri alipoingia nyumbani kwake, akakuta simu za wafanyabiashara wenziye zikiita mfululizo. Akashughulishwa na simu hizo za biashara usiku kucha bila kujali kuwa Ajuza bado alikuwako nje akisubiri koti na shuka.

Asubuhi ya siku iliyofuata, tajiri aliona watu wengi wakizagaa na kushangaa nje ya nyumba yake. Alipotoka akakuta watu wamezunguka maiti ya yule Ajuza ikiwa imeganda kwa baridi.

Kwa bahati Ajuza alimwachia Tajiri ujumbe usemao: "Hata nilipokosa nguo nzito katikati ya baridi kali, bado nilikuwa na USTAHMILIVU WA KIHISIA kwamba nitaishinda baridi. Lakini, ulipoahidi kunisaidia, moyo na akili vilichotwa na matumaini mapya kiasi cha kuua ule USTAHMILIVU WA KIHISIA uliokuwa ndani yangu."

Somo: Usiahidi chochote kwa mtu mwenye uhitaji, ikiwa huna hakika ya kutimiza ahadi yako. Ahadi inaweza kuwa si lolote–si chochote kwako lakini ikawa ni kila kitu kwa mtu uliyemuahidi.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad