Japan na Marekani zimewataka watu wanaoishi kwenye mwambao wa Bahari ya Pasifiki kuelekea sehemu za miinuko, kutokana na kitisho cha Tsunami baada mlipuko wa volkano ya chini ya bahari karibu na Kisiwa cha Tonga.
Picha za satelaiti zimeonyesha mlipuko wa volkano hiyo ya Hunga Tonga-Hunga Ha'apai, ambao umerusha angani moshi na majivu katika umbo la uyoga mkubwa, na kusababisha tetemeko katika eneo la Bahari ya Pasifiki linalokizunguka Kisiwa cha Tonga.
Taarifa za taasisi ya hali ya hewa ya Australia zinasema mawimbi yenye kima cha mita 1.2 yalishuhudiwa katika Mji Mkuu wa Tonga wa Nuku'alofa.
Japan pia imeripoti kuwa mawimbi yaliyotokana na Tsunami hiyo yamefika kwenye pwani yake, yakiwa na kima cha hadi mita tatu.
Hali hiyo imesababisha taharuki na watu wa kisiwa kidogo cha Tonga walionekana wakikimbia mbio kuhamia kwenye maeneo ya vilima.
Mlipuko huo wa volkano ya chini ya bahari ulidumu kwa takribani dakika nane, na umekuja muda mfupi baada ya kutolewa kwa tahadhari ya Tsunami nyingine.