Waziri wa Afya, Ummy leo Januari 26, 2022 amepokea dozi 800,000 za chanjo ya UVIKO-19 aina ya Sinopharm kutoka Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China.
Akizungumza leo Januari 26,2022 mara baada ya kuzipokea chanjo hizo, Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere Dar es Salaam, Ummy Mwalimu aliwataka Watanzania kujitokeza kupata chanzo hizo na kueleza kuwa kiwango kikubwa cha waathirika wa Uviko-19 ni wasiochanja.
Waziri Ummy alieleza kuwa kati ya Septemba 2021 mpaka Januari 23, 2022 watu 76 wamefariki kutokana na ugonjwa wa Uviko-19 kati ya vifo hivyo 73 hawakuchanja. Amesema watu 3147 walilazwa 2990 kati ya hao sawa na asilimia 95 hawakuchanjwa.
Aidha, Waziri Ummy alifafanua kuwa wagonjwa waliokuwa mahututi katika vyumba vya uangalizi maalumu (ICU) Januari 23, 2022 walikuwa 31 kati yao 30 walikuwa hawajachanjwa.
Amesema takwimu zinaonesha mpaka kufikia Januari 25, Watanzania 1,922,019 sawa na asilimia 3.33 walipata chanjo licha ya kukiri kuwa hali hairidhishi katika baadhi ya maeneo nchini.