Timu tano ndogo zilizoshangaza huko Cameroon



Misri ndio mabingwa wa kihistoria wa Afcon ambao wamechukua ndoo mara saba kati ya fainali 24 za mashindano hayo tangu 1957.
YAOUNDE, CAMEROON. WANASEMA kimeumana. Ndio, michuano ya Afcon mwaka huu imekuwa na mambo mengi ya kufurahisha, kuhuzunisha na kushangaza.

Ukizungumzia upande wa mambo ya kushangaza ni viwango vya mataifa mbalimbali ambayo hayakutarajiwa ikiwa yataonyesha viwango hivyo au kufikia hatua walizofikia. Haya hapa mataifa matano ambayo yameshangaza Afcon 2021.

Gambia

Katika kundi la kuwania kufuzu michuano hiyo walimaliza wakiwa vinara kwa alama 10, huku Gabon wakishika nafasi ya pili.

Maajabu yalianzia kwenye hatua hiyo kwa sababu kwenye kundi lao hawakuwa wanapewa kabisa nafasi ya kufuzu kwa sababu ya uwepo wa DR Congo na Gabon. Lakini, baada ya kila taifa kucheza mechi sita msimamo ulikuwa unaionyesha DR Congo na Angola zikishika nafasi ya tatu na nne, huku katika hali isiyotarajiwa Gambia ikawa imemaliza ikiwa kinara wa kundi kwa alama 10.


 
Watu wengi hawakutarajia kuona kilichotokea kwa sababu Gambia na Angola ndizo zilizokuwa zinaonekana timu dhaifu zaidi. Mechi ya kwanza ya hatua ya makundi walicheza dhidi ya Mauritania ambapo walishinda bao 1-0 na katika mechi ya pili walitoka sare ya kufungana bao 1-1.

Katika mchezo wa mwisho waliwafunga Tunisia bao 1-0 na wakamaliza kundi kibabe bila ya kufungwa na kumaliza wakiwa nafasi ya pili kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Baada ya hapo wakafuzu hatua ya 16 bora ambapo waliitoa Guinea. Kwa sasa wapo kwenye hatua ya robo fainali ambapo itacheza dhidi ya wenyeji - Cameroon.

Malawi

Baada ya kuanza fainali za Afcon walikuwa wanatabiriwa watarudi mapema kwa sababu walionekana kuwa miongoni mwa vibonde.

Lakini, katika hali isiyotarajiwa walimaliza kundi wakiwa kwenye nafasi ya tatu wakapita kwa nafasi ya upendeleo kutokana na takwimu zao na baada ya hapo kwenye hatua ya 16 bora walionyesha kiwango bora katika kipindi cha kwanza cha mchezo dhidi ya Morocco, lakini goma lilibadilika kipindi cha pili ambapo Waarabu walipindua meza kwa kusawazisha na kufunga bao la kuongeza kisha wakaibuka na ushindi wa mabao 2-1 na kuiondoa Malawi ambayo ilionekana imeondoka kishujaa kwa sababu hakuna aliyetarajia kama wangefika hatua hiyo.

Comoro

Habari kubwa zaidi wiki hii ilikuwa ni maajabu ya wanajeshi wa Comoro ambao walitolewa kwenye 16 bora na wenyeji Cameroon, Waafrika wameendelea kuwatambua kama mashujaa.

Baada ya kufuzu kiaina kupitia hatua ya makundi ya kuwania kufuzu, lakini kwenye fainali nako watu waliwaona hawana nafasi kwa sababu kundi lao lilikuwa na Morocco, Ghana na Guinea.


 
Maajabu yaliyoje Comoro ikaitoa nishai Ghana kwa kuichapa mabao 3-2 - ushindi ambao uliwasaidia kumaliza nafasi ya tatu na kufuzu hatua ya 16 bora kama moja ya timu zilizomaliza nafasi tatu kwa takwimu nzuri (best looser).

Maajabu waliyoonyesha hatua ya 16 bora ambapo walicheza dhidi ya wenyeji Cameroon. Makipa wao watatu hawakuwa sawa kucheza mechi baada ya kupimwa na kukutwa na maambukizi ya Uviko-19 na sasa mzee mzima Chaker Alhadhur alisimama kwenye milingoti mitatu, huku wasiwasi ukiwa mkubwa kwa sababu nafasi yake asilia ni beki wa pembeni, hivyo, hakuna aliyekuwa anaamini kuwa anaweza kudaka vizuri.

Ha-di dakika 90 zinamalizika wananchi wa Comoro waliokuwa wanashuhudia mechi hiyo bila shaka hawakuwa na cha kuidai timu yao kwa sababu walicheza kwa jasho na damu licha ya kufungwa mabao 2-1 na kutolewa lakini Chaker alifanya kazi kubwa ya kuokoa hatari nyingi.

Cape Verde

Wataalamu hawa walizipiku Rwanda na Msumbiji na kuungana na wenyeji Cameroon kwenye kinyang’anyiro cha kuwania kufuzu mchuano hii.

Cape Verde ambayo ilishindwa kushiriki michuano ya 2019 baada ya Tanzania kuchukua nafasi hiyo sio taifa ambalo lilipewa matumaini ya kufanya lilichofanya.

Kwenye kundi lao katika michuano hii walikuwa kundi moja na Cameroon, Burkinafaso na Ethiopia na kawaida ndio walionekana timu ya itakayomaliza mkiani.

Katika hali isiyo ya kawaida ilifanikiwa kutoka sare na wenyeji Cameroon kisha ikaifunga Ethiopita na kufikisha alama nne ambazo ziliwapeleka katika hatua ya 16 bora kwa tiketi ya timu nne bora zilizomaliza nafasi ya tatu kwenye makundi. Mshangao mkubwa ilikuwa sare na Cameroon ambayo mechi nyingine mbili zote ilishinda.

Sierra Leone

Hawakuwa kundi gumu wakati wanawania kufuzu, kwani walikuwa wanashindana na Benin, Lesotho na Nigeria, hivyo wakafanikiwa kumaliza kundi katika nafasi ya pili kwa alama saba.

Katika michuano yenyewe, Sierra Leone iliishangaza Afrika baada ya kufanikiwa kutoka sare ya bila kufungana dhidi ya bingwa mtetezi Algeria huku kipa Mohamed Kamara ambaye baada ya mchezo huo alionekana akitokwa na machozi.


 
Hawakufanikiwa kufuzu hatua ya 16 bora baada ya kufungwa mechi ya mwisho dhidi ya Equatorial Guinea, lakini ni miongoni mwa timu zilizozua gumzo kutokana na kiwango bora.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad