Try Again Afunguka Simba..Afichua Walivyomrudisha Chama Kininja...Agusia Ishu ya Uwanja na Michango




SIMBA inafanya mambo yake kimya kimya. Ukitaka kudhihirisha hilo ni namna walivyoupiga mwingi kwenye usajili wa kumrejesha kiungo wao Clatous Chama, akitokea RS Berkane ya Morocco.
Uongozi wa timu hiyo, umeamua kuendana na methali ya wahenga inayosema Simba mwenda pole ndiye mla nyama, hii ni baada ya mwenyekiti wa klabu hiyo, Salim Abdallah ‘Try Again’ kuzungumzia mikakati wanayoifanya kimyakimya.

Baada ya usajili wa Chama, Gazeti la Mwanaspoti halikuwa nyuma kuzungumza na Try Again kujua mbinu walizotumia kuzima kelele zilizokuwepo mtaani, zilizokuwa zinamhusisha staa huyo kuwaniwa pia na watani wao Yanga.

MCHAKATO ULIVYOKUWA

Try Again anakiri usajili wa Chama ulikuwa dume, kutokana na namna ilivyotumika nguvu ya ziada kuhakikisha wanawapa kicheko mashabiki wao waliokuwa wakimuimba kila uchao.

Anamtaja mwekezaji wao Mohammed ‘Mo’ Dewji namna alivyoshirikiana nao bega kwa bega kuhakikisha Chama anarejea kwenye chama lake na kuendeleza yale aliyokuwa akiyafanya kabla hajaondoka.

“Chama anaipenda Simba, aliomba arejee kwenye kikosi, maana alikumbuka lile ‘vaibu’ na upendo ambao alikuwa anapewa na mashabiki wake, pia familia yake ilitaka aishi Tanzania na aitumikie Simba,” anasema Try Again na kuongeza:

“Ndio maana hatukuwa na muda na kelele za Chama kuhusishwa na timu nyingine, wakati wanaongea sana, sisi tulikuwa tunafanya vitendo, nadhani mashabiki wetu watakuwa wana raha na kutuamini viongozi wao, maana sasa Chama yuko ndani ya chama,” anasema.

Mbali na Chama, usajili mwingine aliokiri ulikuwa wa kiume ni ule wa Haruna Niyonzima (2017–2019) ambao uligonga vichwa vya watu hadi dakika ya mwisho walipomuona ametinga uzi mwekundu, ndipo upande wa pili Yanga wakapoa.

“Usajili wa Niyonzima haukuwa wa kitoto, mashabiki wetu walikuwa wanataka uhakika wa kujua kama kweli tumemchukua ili kutunza uaminifu kwao, tukafanya kweli, sisi tumezoea kufanya kazi kwa weledi,” anasema na kuongeza kuwa katika uongozi wake ni mkweli na ndio maana anafanikisha jambo analolikusudia.

WATAFANYA HAYA

Anasema kwasababu tayari wana uwanja, pesa watakazozipata zitatumika kujenga majukwaa, gym, hosteli, sehemu za kupoza miili na mengineyo.

“Ndio maana hadi sasa tayari kumefanyika mpango wa kuwapa notisi za kuwataka waondoke wale wote waliovamia eneo la uwanja wa Simba, tumefanya hivyo kwa kuzingatia sheria zinazotakiwa, hivyo Wanasimba wawe na amani kila kitu kitakwenda sawa, maana hao wote waliovamia ni wakati wao kupisha eneo letu,” anasema.

VIPI KUHUSU WAWA

Anasema Simba haina kiburi cha kumuacha beki wao wa kati, Pascal Wawa kiholela wakati bado anahitajika kuisaidia timu na hata siku moja hawataongozwa na tetesi kwa kuwa ni za kawaida kusemwa.

“Wachezaji walikuwa wanatakiwa kutolewa kwa mkopo tumefanya hivyo na wameanza majukumu yao kwenye timu zao, hivyo bado Wawa ni mchezaji wetu, hivi kweli kuna beki kama Wawa kwenye ligi hii,” anasema.

Wachezaji ambao Simba wamewatoa kwa mkopo ni Jeremiah Kisubi (Mtibwa Sugar), Duncan Nyoni na Ibrahim Ajibu alivunja mkataba na amejiunga na Azam FC.

Anasema kwa mtu anayefahamu mpira usajili siku zote ni bahati nasibu ambayo unaweza kupata au kukosa na ndio kilichotokea kwao dhidi ya nyota hao.

“Wote walikuwa wachezaji wazuri lakini muda mwingine wanakosa bahati, mfano Chikwende ni mchezaji mzuri na anacheza timu ya Taifa lakini haikuwa bahati kwake, wakati mwingine bahati pia, ikumbukwe hao wote walisajiliwa chini ya Gomes na sasa huyu ni mwingine,” anasisistiza.

USAJILI WA DIRISHA DOGO

Anawaambia Wanasimba kwamba usajili walioufanya kupitia dirisha dogo ni wa Chama tu, wengine waliokuja kufanya majaribio Etop Udoh, Sharaf Eldin Shiboub na Moukoro Tenena, kocha alikuwa anawaangalia kama watamfaa kwa ajili ya usajili wa dirisha kubwa mwisho wa msimu.

“Ipo hivi, tuna uhusiano mzuri na mawakala wengi, wanatupigia simu kuomba wachezaji wao waje kupata fitnesi kwenye kikosi chetu, pia wachezaji ambao waliwahi kuichezea Simba walituomba waje wafanye majaribio, hivyo hiyo ndio hali halisi,” anasema na kuongeza;

“Sio kila mchezaji anayekuja kufanya majaribio Simba atasajiliwa hapana, ukizingatia kocha alituambia kwamba hataki wachezaji wengi kwenye kikosi chake, anapenda awe na wachezaji ambao watakuwa na ushindani wa kucheza,” anasema na kuongeza kuwa wengine huenda dirisha kubwa wakapata nafasi.

Aidha, Try Again anasema, dirisha dogo kupata mchezaji mzuri ni ngumu sana, licha ya skauti nzuri ambayo wanaifanya na hawakutaka kukurupuka.

USHINDANI WA LIGI KUU

Anasema Ligi Kuu Bara msimu huu imechangamka na imekuwa na ushindani wa kweli, itakayosaidia kumtoa bingwa ambaye atakuwa na ushindani mkali Caf.

“Ligi mara nyingi inapoanza inakuwa kama mbio za nyika, muda unavyoenda wapinzani wanakata upepo, kuna ushindani wa kweli, hilo linatokana na timu kusajili vizuri na kupata mahitaji kwa wakati, jambo ambalo linazifanya zijiandae vyema,” anasema kigogo huyo na kuongeza:

“Nilishasema tunapigana vita vya angani na majini, walikuwa wanatubishia na kuongea maneno mengi, haya vya majini vimetia tiki na tayari tumenyakua taji la Mapinduzi,” anasema.

ISHU YA KAGERA SUGAR

Mtaani inadaiwa Simba iliambiwa na mganga kwamba mechi yao ya Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar iliyopangwa kuchezwa Desemba 18, 2021 wangepigwa 3-0, hivyo wakaamua kuikacha kwa maelezo kwamba nyota wao wengi wanaugua mafua, lakini Try Again anasema Simba haiwezi kuiogopa timu inayoshika mkia.

“Binadamu wameumbwa kusema, lakini ukweli wa mambo wanaufahamu, hivi Kagera iko nafasi ya ngapi mpaka sisi tuiogope? Tumecheza na Yanga, Dodoma Jiji zote ziko juu, ndio tuwaogope Kagera wako nafasi ya mwisho? Sisi kwa bahati mbaya tulikumbwa na maradhi benchi letu la ufundi walikumbwa na ugonjwa.

“Bahati mbaya pia tulikuwa na wachezaji majeruhi kama saba wako Dar es Salaam na hao wagonjwa wakawa zaidi ya 20, katika hali ya kibinadamu unachezaje? Na Bodi ya Ligi na TFF waliona tuna hoja ya msingi na ndio maana waliamua kuahirisha mechi.

“Halafu sisi tumetumia pesa nyingi kukodi ndege hapa hadi Bukoba, sasa tuahirishe mechi kisa Kagera Sugar, sio kweli hata kidogo na tutatumia gharama nyingine tena kurudi kucheza nao tena,” anasema.

URAIS WA MO

Anasema ndani ya miaka minne ambayo Mo Dewji alikuwa mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi, amefanikiwa kunyakua mataji manne mfululizo ya Ligi Kuu na kufanya vyema kimataifa.

“Matunda ya Mo Dewji yapo wazi, tulichukua mataji yote kasoro mwaka jana hatukufanikisha Mapinduzi, tumefika mbali michuano ya Caf, wamesajiliwa wachezaji ghali, hadi hapo hastahili kuwa rais wa heshima?” anahoji.

Anaendelea kusimulia: “Hatuna maana kwamba viongozi wengine waliotangulia hakuwa na mchango mkubwa, ila nimefafanua wanaohoji hayo mambo,” anasema.

Kuhusu Mo kuacha kutoa bonasi kama zamani, Try Again anasema, kila kitu kinaendelea kama ilivyokuwa nyuma japokuwa hayupo katika nafasi yake.

“Kila mtu atasema lake, lakini timu ambayo haina morali inaweza kufanya vizuri kama Simba inavyofanya kwenye ligi na kutwaa taji la Mapinduzi? Hizo ni propaganda tu ambazo hauwezi kuwazuia watu kusema.”

MICHANGO YA MASHABIKI

Anasema walisitisha kwa muda kuhamasisha kuwachangisha mashabiki baada ya kuelekeza nguvu kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi.

“Kwa sasa tunaendelea kama kawaida na utaratibu wa hamasa, kama siku ya kwanza tu, tulivyofungua zoezi la uchangishaji kuanzia saa 9 mpaka 12 jioni mashabiki walichangia Sh17 milioni, unaweza ukaona watu wana mwamko wa kiasi gani,” anasema.

Anaulizwa hadi sasa kimekusanywa kiasi gani? Anajibu kuwa; “Hilo lipo chini ya mtendaji mkuu Barbara Gonzalez ndiye ametunza hizo hesabu hivyo muda ukifika kila kitu kitawekwa sawa na hapo tutaangalia na hali ya fedha itakavyokuwa ndio tutaandaa ramani na michoro.”
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad