UKISIKIA jeuri ni hii ambayo wameifanya mabosi wa Yanga ambapo kwa sasa wanasubiria muda tu kwa ajili ya kumtambulisha kiungo mshambuliaji wa Zanaco ya Zambia, Moses Phiri.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo Championi Jumamosi limezipata ni kuwa tayari wamemalizana na kiungo mshambuliaji, Moses Phiri na tayari amesaini mkataba wa awali wa kujiunga na timu hiyo.
Mabosi hao wamepanga kumtambulisha staa huyo mapema Juni, mwaka huu ambao utakuwa wakati wa dirisha kubwa ikiwa ni baada ya kutajwa staa huyo kumalizana na Wanajangwani hao.
Mmoja wa mabosi wa Yanga, ameliambia Championi Jumamosi kuwa, ni suala la muda Phiri kutua katika timu hiyo baada ya taratibu zote kukamilika za kumsajili kutoka klabu yake ya Zanaco ambayo imeridhia kumuachia.
Bosi huyo alisema kuwa, kama timu yake itaondolewa mapema katika Kombe la Shirikisho Afrika, basi haraka atajiunga na Yanga, lakini uhakika atajiunga na Yanga Juni, mwaka huu kipindi ambacho dirisha la usajili limefunguliwa kwa ajili ya msimu ujao.
“Phiri mwenyewe pamoja na meneja wake ndiyo wameomba kujiunga na Yanga Juni, mwaka huu wakati dirisha la usajili la msimu ujao litakapofunguliwa.
“Na kikubwa yeye ameomba kucheza Kombe la Shirikisho Afrika kwa ajili ya kujitangaza na kuongeza thamani yake katika michuano hiyo mikubwa Afrika.
“Hivyo uongozi wa Yanga uliosafiri kwenda Zambia, ulikubali licha ya kumpa sharti la kusaini mkataba wa awali wa ajira wa miaka miwili ambao utambana kwenda kusaini sehemu nyingine yoyote,” alisema bosi huyo.
Awali staa huyo aliweka wazi kuwa klabu yake ilifanya mazungumzo na timu hiyo ya Yanga lakini kwake bado hajasaini mkataba na anatarajia kutua nchini mwezi huo Juni.
“Uhakika kabisa wa kuja Tanzania ni mwezi Juni mwaka huu kwa sababu kwa sasa haiwezekana mpaka mwisho mwa msimu. Naamini kila kitu ni mipango, hivyo sina sana haraka.”