Ni siku mbili tu tangu aliyekuwa Spika wa Bunge la Jumhuri wa Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, akabidhi barua ya kujiuzulu kwa Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Daniel Chongolo.
Tangu kukabidhi barua hiyo, picha na video za aliyekuwa Naibu wake, Tulia Akson (Mbunge Mbeya Mjini) zimekuwa zikisambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii.
Times FM Radio ilizungumza na mchambuzi wa masuala ya kisiasa na uchumi, Nassor Kitunda, ambaye alisema upo uwezekano mkubwa wa Tulia Akson kirithi kiti hicho.
"Kwa vyovyote vile Tulia Akson atagombea nafasi hiyo kwa sababu kwanza ana uzoefu lakini pia ni ndoto ya kila mtu kushika madaraka ya juu ya eneo lake," alisema.
Kutokana na uchambuzi huo, Times FM, iliwasiliana na Mwanasheria Jebra Kambole, kujua kisheria kama Naibu Spika huyo anaweza kuvaa viatu vya Ndugai.
"Naibu Spika Tulia Akson anayo nafasi ya kuweza kugombea kiti hicho lakini lazima kwanza aachie nafasi ya u-Spika ili anapokwenda kugombea kiti hicho asiwe na kofia nyingine yoyote," alisema Kambole na kuongeza:
"Sasa anapokwenda kugombea akiwa hana kofia yoyote ikiwemo ya u-Naibu Spika anaweza kushinda au asishinde hivyo akajikuta Unaibu Spika wake pia unapotea."