Upinzani TZ washangilia kujiuzulu kwa Spika aliyekosoa Rais Suluhuq



UPINZANI nchini Tanzania umesherekea kujiuzulu kwa Spika wa Bunge Job Ndugai ambaye aling’atuka baada ya kumkosoa Rais Samia Suluhu Hassan.

Naibu Mweyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tundu Lissu jana alidai kuwa spika huyo alitumiwa na serikali kukandamiza wanasiasa wa upinzani bungeni.

Ndugai alikosana na Rais Suluhu wiki iliyopita baada ya kumkosoa kwa kukimbilia kukopa hela kutoka mataifa ya kigeni.

Ndugai ambaye ni mbunge wa Kongwa, alisema kuwa Tanzania huenda ikapigwa mnada iwapo itaendelea kukopa madeni kutoka mataifa ya kigeni bila kikomo.

Kauli hiyo ilionekana kumgadhabisha Rais Suluhu ambaye alishikilia kuwa serikali yake itaendelea kukopa hela kwa ajili ya miundomsingi.

Rais Suluhu alisema kuwa wakosoaji wake waliongozwa na tamaa ya kutaka kumpokonya urais katika uchaguzi wa 2025.

Wandani wa Rais Suluhu walimtaka Ndugai kujiuzulu kwa ‘kumkosea heshima’ kiongozi wa taifa hilo la Afrika Mashariki.


Ndugai alijiuzulu siku chache baada ya kuomba msamaha Rais Suluhu na Watanzania kwa ulimi wake ‘kuteleza’.

Vikao vya bunge vilisitishwa hadi pale spika mpya atachaguliwa mwishoni mwa mwezi huu.Hiyo ni mara ya kwanza kwa spika aliye madarakani kujiuzulu kwa hiyari yake katika historia ya bunge la vyama vingi nchini Tanzania.

Baadhi ya wadadisi wanasema kwamba kinachoendelea sasa kinaonyesha mgogoro wa madaraka ndani ya chama tawala cha Mapinduzi (CCM).

“Spika Ndugai katika historia yetu yote ya kibunge hatujawahi kuwa na Spika wa hovyo na ambaye amevuruga Bunge na kulifanya kuwa chombo kinachotumikia Ikulu kuliko Spika yeyote,” Bw Lissu alidai jana.

Bw Lissu alidai kuwa Rais Suluhu ameanza mchakato wa kuwatimua wandani wa mtangulizi wake Hayati John Pombe Magufuli aliyeaga dunia Aprili 2021.

“Tangu Bunge letu lianzishwe mwaka 1926 takribani miaka 96 iliyopita haijawahi kutokea spika amelazimishwa kujiuzulu kwa namna ambayo spika Ndugai amelazimika kujihuzulu hapo jana.

“Spika Ndugai alikuwa kibaraka wa Hayati John Magufuli kwa kipindi chote alichokuwa Spika. Inaonekana Rais Samia ameanza kufurusha vibaraka wa Magufuli,” alisema Lissu.

Upinzani, wakati huo huo, umetumia masaibu ya Ndugai kufufua mjadala wa kudai katiba mpya utakaopunguza mamlaka ya Rais.

“Kulazimishwa kwa Spika Ndugai kujiuzulu kunathibitisha wazi kabisa kile ambacho tumekisema kwa miaka mingi, kwamba kwa mfumo wetu wa kikatiba umempa Rais mamlaka mengi kupita kiasi.

“Tupate katiba mpya ili Bunge liwe kweli chombo cha uwakilishi cha wananchi badala ya kuwa chombo cha kupiga muhuri maamuzi yanayofanywa na Rais. Katika historia ya nchi yetu maamuzi karibu yote yamekuwa yakifanywa na Ikulu halafu Bunge linapiga muhuri tu,” akasema Lissu.

Rais Suluhu alipochukua hatamu za uongozi kufuatia kifo cha Magufuli kulikuwa na matumaini makubwa kwamba angefungua demokrasia na uhuru wa vyombo vya habari.

Lakini Rais Suluhu amekuwa akikosolewa kwa kuendelea kugandamiza upinzani. Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe amekuwa akizuiliwa tangu Julai 2020 kwa madai ya kuhusika na ugaidi lakini upinzani unasema hiyo ni njia ya kuwatishia.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad