Dodoma/Mbeya. Uamuzi wa CCM kumteua Mbunge wa Mbeya Mjini, Dk Tulia Ackson kugombea nafasi ya Spika wa Bunge umewaweka katika wakati mgumu wapinzani wake ndani ya chama hicho na wale wa vyama vingine katika kulirudisha jimbo hilo mikononi mwao.
Tangu mwaka 2010 hadi 2020 jimbo la Mbeya Mjini lilikuwa chini ya Chadema, likiongozwa na Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ na kwa kipindi hicho ilionekana ni ngome ya chama hicho.
Hata hivyo, katika Uchaguzi Mkuu wa 2020, jimbo hilo lilirudi CCM baada ya mgombea wake, Dk Tulia kutangazwa mshindi kwenye uchaguzi uliolalamikiwa na wapinzani kuwa ulitawaliwa na rafu nyingi.
Baadhi ya wachambuzi wanaona kama Dk Tulia atashinda katika hatua ya mwisho na kuwa Spika, huenda akaongeza nguvu ya kuendelea kulishika jimbo hilo katika chaguzi zijazo.
Kumbukumbu zinaonyesha walioshika nafasi ya Spika kuanzia Pius Msekwa, Samuel Sitta na Job Ndugai haikuwa rahisi kwa wapinzani wao ndani na nje ya chama chao kuwang’oa katika nafasi ya ubunge.
Akizungumzia hatua hiyo, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mbeya, Joseph Mwasote ‘China’ alisema kitendo cha CCM kumteua Dk Tulia kuchukua nafasi ya Spika wa Bunge kinalenga kudhoofisha upinzani kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, lakini hawatakubali.
Hata hivyo, alisema wanasubiri, ili katika uchaguzi mkuu ujao waone wanajipanga vipi.
“Ufike wakati Serikali itambue kitendo cha kuua upinzani kitarudisha nyuma maendeleo. Ni vema kuheshimiwa kwa misingi ya demokrasia, ili vyama vya siasa vifanye kazi kwa uhuru,” alisema.
Pamoja na hayo, kwa upande mwingine imeelezwa hatua ya Dk Tulia kuwa Spika wa Bunge inaweza isimsaidie kisiasa kama chaguzi zitakuwa huru na za haki.
Hoja hiyo inaungwa mkono na mifano ya baadhi ya waliokuwa viongozi wa juu serikalini, lakini walishindwa majimboni.
Mfano aliyekuwa Waziri Mkuu na Makamu wa kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Joseph Warioba aliyeshindwa kwenye ubunge na mpinzani, Steven Wassira, wakati huo Warioba akiwa Waziri wa Tamisemi.
Pia, aliyekuwa mbunge wa Mtera kwa sasa jimbo la Mvumi, John Malecela alivuliwa ubunge baada ya kushindwa kwenye kura za maoni ndani ya CCM na Livingstone Lusinde ambaye ni mbunge hadi sasa.
Malecela mbali na nafasi nyingine za uongozi, pia alikuwa Waziri Mkuu na Makamu wa kwanza wa Rais.
Akizungumzia suala hilo, mchambuzi wa masuala ya siasa, Bubelwa Kaiza alisema nafasi ya uspika inaweza isimsaidie Dk Tulia jimboni humo.
“Siamini kwamba nafasi ya uspika itampa nguvu jimboni kwa sababu nafasi hiyo ni vyeo vya bungeni tu kama uenyekiti na vyeo vingine,” alisema Bubelwa.
Huku akitaja maspika waliopita, Bubelwa alisema uspika haukusaidia kuleta maendeleo kwenye majimbo ya maspika hao.
“Watu wanataka barabara, maji, huduma za afya na elimu. Kwa hiyo sidhani kama itamsaidia sana Dk Tulia jimboni kwake. Tena asipoangalia ndiyo itamharibia kabisa,” alisema.
Maspika wengine
Anne Makinda, aliyekuwa mbunge wa Njombe Kusini mkoani Njombe alikaa kwenye nafasi ya Spika kwa awamu moja ya miaka mitano kuanzia 2010 hadi 2015. Hata hivyo, hakugombea ubunge akiwa Spika. Msekwa alikuwa Spika wa Bunge kuanzia mwaka 1994 hadi 2005 aliposhindwa kinyang’anyiro hicho ndani ya CCM na Samuel Sitta.
Kwenye nafasi ya ubunge wa jimbo la Ukerewe mkoani Mwanza mwaka 2000 alishindwa kwenye kura za maoni ndani ya CCM na Getrude Mongella, lakini alikwenda kugombea nafasi ya Spika na alishinda na kuwa Spika asiyekuwa mbunge. Msekwa aliondolewa kwenye nafasi ya Spika baada ya kushindwa kwenye kura za kamati ya wabunge wa CCM na Samuel Sitta aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Urambo mkoani Tabora.
Sitta alikaa kwenye nafasi ya Spika kwa awamu moja ya kuanzia 2005 hadi 2010 na kwenye ubunge aliliacha jimbo kwa Margareth Sitta ambaye ni mkewe.
Ndugai alikuwa Spika kuanzia mwaka 2015 na kwenye Uchaguzi Mkuu 2020 alipita bila kupingwa kuanzia ndani ya CCM hadi jimboni.
Kwa Dk Tulia kama atachaguliwa kuwa Spika wa Bunge, sehemu pekee wanayoweza kumwangusha ni ndani ya CCM.
Kwa upande mwingine, akizungumza na Mwananchi jana, Mwenyekiti wa Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Geoffrey Mwandulusya alisema kuwa wana kila sababu kuunga mkono uteuzi huo kwa lengo la kutaka Mbeya kupiga hatua za kimaendeleo na kuachana na propaganda za kisiasa.
Mwandulusya, ambaye pia ni Mwenyekiti wa shirikisho la vyama vya siasa Mbeya, alisema kuwa kwa kutambua Dk Tulia licha kuwa Mbunge wa Mbeya pia ni Mhimili wa Bunge, umefika wakati wa kuungana kwa lengo la kuleta maendeleo ya kweli katika jimbo hilo.