Utaratibu wa kung’oa Spika madarakani



Job Ndugai Spika wa Bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania
WAKATI joto la kuachia madaraka kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai likiendelea kushika kasi, Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Juni 2020, zimebainisha utaratibu kumng’oa endapo hatojiuzulu kwa hiari. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Hayo yanajiri katika kipindi ambacho Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akimkosoa vikali hadharani kiongozi huyo wa muhimili wa Bunge, juu ya kauli aliyoitoa kuhusu mkopo wa Sh.1.3 trilioni, kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF).

Mkopo huo ulikuwa na lengo la kuchochea mapambano dhidi ya UVIKO-19 kwa kuelekeza kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya afya, elimu, miundombinu ya barabara pamoja na maji.

Spika Ndugai alisema, umefika wakati Serikali ikaacha kukopa na kujibana kwenye makusanyo ya ndani ikiwemo kutumia fedha za tozo huku akisema, endapo madeni yakizidi nchi inaweza kupigwa mnada.


 
Jana Jumanne, tarehe 4 Januari 2022, Rais Samia alimtolea uvuvi Spika Ndugai akimweleza anachokifanya ni homa ya uchaguzi mkuu 2025.


Kutokana na kauli hiyo ya Rais Samia ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinachoongoza serikali, kimemweka katika wakati mgumu Ndugai kuendelea kuwa Spika.

Duru za siasa zinaeleza, anachopaswa kukifanya kwa sasa kujiuzulu nafasi hiyo na kama atashindwa, miongoni mwa wabunge wanaweza kutumia kanuni za Bunge, kumng’oa.


Kifungu cha 158 kipengele cha kwanza hadi cha sita, kinaeleza utaratibu unaoweza kutumia kumng’oa spika madarakani.

Vipengele hivyo ni;

1. Mbunge yeyote anayetaka kuwasilisha hoja ya kumwondoa Spika madarakani chini ya Ibara ya 84(7) (d) ya Katiba, atawasilisha taarifa ya maandishi ya kusudio hilo kwa Katibu akieleza sababu za kutaka kuleta hoja hiyo.

2. Mara tu baada ya kupokea taarifa ya maandishi ya kusudio la kumwondoa Spika kwenye madaraka, Katibu ataipeleka taarifa hiyo kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa ajili ya kuijadili.

3. Endapo Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge itaridhika kuwa zipo tuhuma mahsusi dhidi ya Spika zinazohusu uvunjaji wa masharti ya Ibara ya 84(7) (a), (b), (e), (f), (g) na (h) ya Katiba, Sheria au Kanuni zinazoongoza shughuli za Bunge, basi Kamati hiyo itaidhinisha kuwa hoja hiyo ipelekwe Bungeni ili iamuliwe.

4. Naibu Spika, atakalia Kiti cha Spika wakati wa kujadili hoja ya kutaka kumwondoa Spika madarakani na Spika atakuwa na haki ya kujitetea wakati wa mjadala.

5. Spika atakuwa ameondolewa kwenye madaraka endapo zitapigwa kura zisizopungua theluthi mbili ya idadi ya Wabunge wote za kuunga mkono hoja hiyo na uamuzi wa Bunge utafanywa kwa kuzingatia kura za siri.

6. Spika anayetuhumiwa anaweza kujiuzulu nafasi yake kwa kutoa maelezo ya kujiuzulu kwake Bungeni kabla ya uamuzi juu ya hoja ya kumwondoa madarakani.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad