SERIKALI imerejesha utaratibu wa kuwaunganisha watanzania na ajira nje ya nchi kuanzia juzi.
Taarifa iliyotolewa juzi jioni na Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu ilisema serikali imerejesha utaratibu huo ili kutoa fursa kwa watanzania wenye shauku na sifa kufanya kazi nje ya nchi.
“ Kwa kutambua mchango mkubwa wa fursa za ajira zinazopatikana nje ya nchi katika maendeleo ya nchi yetu, na kwa kuzingatia kuwa, tunao Mwongozo kwa Mawakala Binafsi unaobainisha masuala ya msingi katika kuunganisha watanzania na fursa za ajira nje ya nchi.
“ Tunapenda kuufahamisha umma wa Watanzania hususani Wakala Binafsi wa Huduma za Ajira pamoja na Watanzania wenye shauku na sifa ya kufanya kazi nje ya nchi kuwa, shughuli za kuunganisha Watanzania na fursa za ajira nje ya nchi kupitia Mawakala Binafsi wa Huduma za Ajira zinarejeshwa rasmi kuanzia leo (juzi) kwa kuzingatia Sheria, Kanuni pamoja na Mwongozo Mpya.”
Julai 2018, Waziri mwenye dhamana ya masuala ya kazi na ajira alisitisha huduma ya kuunganisha Watanzania
na fursa za ajira nje ya nchi kupitia Mawakala Binafsi wa Huduma za Ajira. Hatua hii ilitokana na ukiukwaji mkubwa wa sheria na kanuni uliokuwa ukifanywa na baadhi ya Mawakala.
Pia Serikali ilichukua hatua hizo ili kuweka utaratibu mzuri utakaowezesha Watanzania kunufaika zaidi na fursa za ajira nje ya nchi.
“ Hivyo basi, tunawajulisha Wakala Binafsi wa Huduma za Ajira nchini ambao wamepata fursa za ajira kwa Watanzania nje ya nchi kuwasilisha maombi yao kwa Mkurugenzi wa Huduma za Ajira (TaESA) ili waweze kupatiwa vibali vya kuunganisha watanzania na fursa husika” ilisema taarifa hiyo.
Aidha, Serikali imesema inatambua na kuzingatia kuwa katika kutumia fursa za ajira nje ya nchi usalama na haki za msingi kwa Watanzania ni suala lisilo na mbadala na hivyo ni lazima uunganishaji wa watanzania na fursa za ajira nje ya nchi uzingatie viwango vya kazi za staha vinavyokubalika na Shirika la Kazi Duniani (ILO).
Taarifa hiyo imesema kwa wale wasio na leseni na wana fursa za ajira nje ya nchi wawasilishe maombi ya leseni kwa Kamishna wa Kazi yakiambatana na ada ya usajili ya kipindi cha mwaka mmoja isiyorudishwa kiasi cha Sh 500,000.