TAHARUKI: Familia zilizopotelewa na ndugu zao watano katika mazingira ya kutatanisha tangu Desemba 26, 2021 maeneo ya Kariakoo ‘Kamata’ wamepanga kuonana na Waziri wa Mambo ya Ndani awasaidie.
Kwa mujibu wa familia hizo, wamefikia hatua hiyo baada ya kushindwa kupata msaada kutoka kwa Jeshi la Polisi tangu waliporipoti jambo hilo Desemba 27, 2021.
Waliopotea ni Tawfiq Mohamed, Self Swala, Edwin Kunambi, Hemed Abass na Rajabu Mdoe.
Badhi ya ndugu wa waliopotea walisema leo wanatarajia kufanya kikao cha pamoja ambacho ni maandalizi ya kwenda kumuona Waziri wa Mambo ya Ndani.
Naye Sylvia Quentin ambaye ni Mama mzazi wa Tawfiq Mohamed, alisema siku ya mwisho mmoja wao alituma ujumbe mfupi wa simu (sms) kuwa wamekamatwa eneo la Kariakoo wakiwa kwenye gari aina ya Toyota IST nyeusi na wanapelekwa Kituo Kikuu cha Polisi.
Alisema baada ya kupata taarifa hizo ndugu hao walianza kuwafuatilia, ikiwamo kuzunguka kwenye vituo vingine vya polisi bila mafanikio, ndipo walianza kuzungukia kwenye hospitali mbalimbali katika vyumba vya kuhifadhia maiti, hata hivyo hawajawapata ndugu zao.
Kamanda wa polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amekiri kupata taarifa hizo na kuongeza kuwa polisi kwamba wanaendelea kuchunguza na kuwatafuta.
“Hao watu walishafika na stori hizo nilishazisikia, waliniambia walikuwa watano, si kwamba kila anayepotea anakuwa amechukuliwa na Polisi na si kila anayepotea anakuwa amekufa, mara ngapi watoto wanapotea na baadaye wanaonekana? Kwa hiyo mtu akipotea utulivu unahitajika,” alisema.