Viongozi CHADEMA watumbuliwa



CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kimevunja uongozi wa wake Wilaya ya Mbeya Mjini kutokana na wajumbe wake kufanya makosa mbalimbali ikiwamo kuvuruga mkutano wa kanda hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za chama hicho Kanda ya Nyasa, Mwenyekiti wa Kanda hiyo, Mchungaji Peter Msigwa, alisema viongozi walioondolewa kwenye uongozi huo wapo 11 wakiongozwa na Mwenyekiti John Mwambigija.

Alisema viongozi hao waliongoza genge la wahuni kufanya fujo kwenye mkutano wa chama hicho kanda uliokuwa na lengo la kusuluhisha mgogoro uliokuwapo kati ya viongozi hao na wanachama.

Msigwa alisema wanachama wa CHADEMA Jimbo la Mbeya Mjini walikuwa wanawalalamikia viongozi hao kuwa wanawafukuza uwanachama bila kufuata utaratibu na waliwafukuza baadhi ya viongozi waliochaguliwa na wananchi.

Alisema baada ya taarifa za mgogoro huo kuufikia uongozi wa chama hicho kanda pamoja na maelekezo ya Taifa iliamuliwa Kamati Tendaji ya Kanda hiyo kwenda kusuluhisha na wakati mkutano wa usuluhishi unaendelea ndipo Mwambigija na wenzake walianzisha fujo.


 
Alisema kutokana na kufanya fujo hizo, kamati hiyo iliamua kuahirisha mkutano na ndipo vikafanyika vikao ambavyo viliamua wavuliwe uongozi na wabaki kuwa wanachama wa kawaida wakati taratibu zingine zikiendelea.

“Kwa mujibu wa taratibu za chama chetu maamuzi ya kinidhamu yanaanzia kwenye ngazi za chini na hawa walitakiwa washughulikiwe na ngazi ya mkoa, lakini tumechukua hatua hizi ngazi ya kanda kwa sababu walionyesha utovu wa nidhamu kwenye mkutano wa ngazi yetu,” alisema Msigwa na kuongeza.

“Mbali na kuwavua uongozi, tumewaandikia barua za kuwataka wajieleze ndani ya siku 14 kwanini wasifukuzwe uwanachama kutokana na vitendo vyao vya utovu wa nidhamu,” alisema Msigwa.


Vilevile Msigwa alisema Kamati Tendaji ya Chama hicho Kanda ya Nyasa imeuelekeza uongozi wa chama hicho Mkoa wa Mbeya, kuunda kamati maalumu ndani ya siku tatu ambayo ndiyo itakuwa inaendesha shughuli za chama hicho katika wilaya hiyo.

Hata hivyo, alisema Kamati hiyo Tendaji ya Kanda iliuelekeza uongozi wa CHADEMA ngazi ya Mkoa wa Mbeya kuandaa uchaguzi wa kuziba nafasi za viongozi hao ndani ya siku 60 muda ambao alisema ni kwa mujibu wa katiba ya chama hicho.

Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Mbeya, Joseph Mwasote maarufu China wa China, alisema katika mkoa huo kuna majimbo saba, lakini lenye mgogoro ni la Mbeya Mjini pekee ambalo alisema limekuwa likiwaumiza vichwa.

Alisema wao wasingeweza kufanya maamuzi ya kinidhamu dhidi ya viongozi hao baada ya kufanya fujo hizo kwa sababu kikao hicho hakikuwa katika ngazi yao.

Alisema tukio walilolifanya viongozi hao liliwafedhehesha kutokana na kwamba wao ndio walikuwa wenyeji wa mkutano huo na kwamba walijiandaa toka mwanzo kwa kuhakikisha wanachama waliowafukuza hawaingii.

Kwa upande wake mwenyekiti aliyeondolewa kwenye nafasi yake, Mwambigija alisema yeye hatambui maamuzi ya viongozi wa Kanda na hivyo yeye bado ni mwenyekiti wa Chama Wilaya ya Mbeya Mjini na bado anaendelea kufanya shughuli za chama.

“Mimi bado ni Mwenyekiti wa CHADEMA Mbeya Mjini na kesho (leo) nitakuwa na mkutano na wajumbe wa Kamati Kuu ya Wilaya, hawa wanaotangaza kunivua uongozi kwenye vyombo vya habari wamechemka,” alisema Mwambigija.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad