Wadau watoa maoni kauli ya Samia



BAADHI ya wachambuzi na wadau wa siasa, wametoa maoni kuhusu kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan, huku wakisema inaonyesha msimamo thabiti na kwamba ana mamlaka hayo.

Hata hivyo, baadhi wameshauri kwamba ni wakati wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kukutana na kujadiliana kuhusu suala la Spika Job Ndugai, kuhusu kauli yake ya mikopo.

Juzi Rais Samia alisema kuna baadhi ya watu wamekuwa wakijipanga kwa ajili ya mbio za urais mwaka 2025 na kusahau utekelezaji wa majukumu yao, hivyo anakusudia kuwaondoa ili wakaendelee na harakati zao. Pia alisema hata kauli za baadhi ya viongozi zinatokana na joto la urais 2025,

Wakizungumza jana na Nipashe kwa nyakati tofauti, wachambuzi hao walisema kuna uhusiano mkubwa kati ya chama na serikali na kwamba kutofautiana kimantiki ndani ya chama kikubwa ni kawaida ingawa huhatarisha afya ya kisiasa, hususan utekelezaji wa majukumu yaliyopangwa.

Abbas Mwalimu, mchambuzi wa masuala ya kisiasa, alisema kauli aliyoitoa Rais juzi, inatokana na mamlaka aliyo nayo na taasisi anayoiendesha, Ikulu, inayobeba masuala yote ya kiutendaji na utekelezaji wa dira na mipango ya maendeleo ya taifa.


 
“Ikulu ni taasisi iliyo na jukumu la kubeba maono ya kiongozi aliyepo. Maono ya Rais Samia ndiyo ya taasisi ya sasa inayotekeleza mpango wa maendeleo na dira ya taifa. Ibara ya 33 ya Katiba inampa mamlaka ya kuamuru, Rais ni Mkuu wa nchi na Amiri Jeshi Mkuu, anatoa amri.

“Ili kufikia ustawi wa wananchi, unahitajika uratibu, sera zitekelezeke na zinaundiwa sheria, huko bungeni. Kama kuna changamoto hapo maana yake kuna tatizo,” alisema Mwalimu.

Naye, mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Gwandumi Mwakatobe, alisema ili kulinda afya ya chama (CCM), ambacho anakitaja ni kikubwa na maarufu barani Afrika, suala la kutofautiana kimsimamo ni la kawaida.


“Ni kawaida chama kikubwa kuwa na mitazamo tofauti na pengine hili lilitegemewa kama alivyosema Rais kwamba ni homa ya uchaguzi 2025. Ingawa ninafikiri ni wale ambao walikuwa wakijiandaa na urais kabla hata ya yeye kuingia mamlakani, bado wana ari hiyo.

“Tatizo la Ndugai si hoja yake, yeye ndiye anapitisha fedha bungeni. Tozo amepitisha bungeni leo anasema mikopo haifai. Hajatoa njia ambayo nchi ili ijitegemee ifanye nini. Yeye angezungumza na mhimili mwingine kupata maoni kabla ya kuzungumzia mikopo,” alisema Gwandumi.

Juzi, rais Samia alisema atafanya mabadiliko hivi karibuni katika nafasi mbalimbali ndani ya serikali yake, ikiwamo baraza la mawaziri, ili kuondoa waliojiingiza kwenye makundi ya kuwania urais mwaka 2025, ili apate nafasi ya kuwateua watu watakaomsaidia katika kuiongoza serikali kuwatumikia Watanzania.

Alisema safu za uongozi ndani ya CCM, zikiwamo za ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na wenyeviti wa ngazi mbalimbali, zimeanza kuandaliwa lengo likiwa kujipanga kwa ajili ya urais.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad