Wakati Yanga Wakienjoy SOKA La Pasi Sambusa, EL Merrikh ya Sudan Wamtaka Tena Kocha Nabi..Ishu Iko Hivi

 


VINARA wa Ligi Kuu, Yanga jana jioni walikuwa uwanjani kumalizana na maafande wa Polisi Tanzania, huku nyuma kuna taarifa ya kushtua kwa mashabiki wa klabu hiyo kuhusu kocha Nasreddine Nabi aliyeibadilisha timu na kucheza shoo shoo.

Kocha huyo alipata wakati mgumu wakati anaanza kibarua chake Jangwani kabla ya kupenyeza falsafa zake zinazoifanya sasa Yanga kucheza soka tamu la pasi nyingi na kushambulia sana, huku ikigawa dozi kwa wapinzani ndani ya ligi.


Hata hivyo, taarifa ni kwamba kocha huyo anatarajiwa kumaliza mkataba wake Juni 30 mwaka huu na hadi sasa huku ikielezwa tayari mezani mwake ana ofa tatu kutoka nje ikiwamo klabu yake ya zamani ya El Merrikh ya Sudan.


Mbali na kocha huyo mkataba wake kuelekea ukingoni, lakini hadi sasa hakuna mazungumzo yoyote yaliyoanza baona ya Nabi na mabosi wa klabu hiyo.


Inafahamika kuwa tayari Nabi amepokea ofa zaidi ya timu tatu kutoka nje ya nchi ikiwamo El Merrikh aliyokuwa akiinoa kabla ya kupigwa chini mapema mwaka jana akiwa ameitumikia kwa muda wa siku 38 tu na kutua Jangwani.


Akizungumza Nabi alisema kwa kocha yeyote anayefanya vizuri katika timu anayofundisha, lazima kutakuwa na nyingine zinazomhitaji na anategemea hilo hata kwa upande wake.


Nabi alisema kuhusu suala la kumalizika kwa mkataba wake ni makubaliano ya pande mbili muajiri na muajiriwa, hivyo kama unamalizika muda ukifika bila kuongezewa mwingine hapo ndio itajulikana.


“Hahaha! Nyie mnachunguza sana. Haya sawa ngoja kwanza tuna mechi ngumu mbele yetu tumewekeza nguvu zaidi, lakini jambo la mkataba wangu kuelekea ukingoni mpo sahihi,” alisema Nabi na kuongeza kuwa, mara nyingi kocha, mchezaji au muajiriwa mkataba wake unapobaki miezi sita kumalizika kunakuwa na mazungumzo ya kumuongezea mpya ila mpaka sasa kwake hakuna.


SIO NABI TU


Hata hivyo, ndani ya Yanga si Nabi peke yake ambaye mkataba wake unaelekea ukingoni bali kuna wachezaji ambao msimu huu ukimalizika mikataba yao nayo itakuwa imekwisha.


Wachezaji hao ni nahodha wawili, Bakar Mwamnyeto, beki Kibwana Shomary na Saido Ntibazonkiza.


Hata hivyo, Mjumbe wa Kamati ya Usajili Yanga, Injinia Hersi Said alipoulizwa kuhusu ya suala la kumalizika kwa mkataba wa kocha wao Nabi na baadhi ya nyota wa kikosi hicho, alisema wanalifahamu hilo, lakini kwa wakati huu wamewekeza nguvu kwanza kufanya vizuri katika mechi za ligi kisha mengine yatafuata.


“Hata kwa wachezaji wanaomaliza mikataba yao tunalifanyia kazi na baada ya kila kitu kwenda sawa ikiwamo kwa kocha tutayaweka wazi kama utaratibu wa klabu ulivyo,” alisema Injini Hersi kuhusu mipango ya miamba hiyo ya Jangwani.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad