Imam Mogaeka kutoka shule ya Feza Boys ambaye ameingia kwenye 10 bora kitaifa matokeo ya kidato cha nne
Dar es Salaam. Wanafunzi wawili wa shule za Feza walioingia kwenye orodha ya wanafunzi 10 bora kwenye matokeo yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani (Necta) wamewashukuru walimu wao kwa ushirikiano na mafunzo waliyowapatia.
Wanafunzi hao ni Imam Mogaeka kutoka shule ya Feza Boys ambaye ameingia kwenye 10 bora kitaifa kidato cha nne na Loi Kitundu kutoka Feza Girls ambaye ameingia kwenye 10 bora matokeo ya kidato cha pili.
Wakizungumza na vyombo vya habari leo Jumamosi Januari 15, 2022 wanafunza hao wameeleza kwamba haikuwa rahisi kwao kuingia kwenye orodha ya 10 borakwa sababu wanafunzi wengi wana uwezo.
Mhitimu Imam Mogaeka amesema amepokea matokeo hayo kwa mshituko kwa sababu hakurajia kama angeingia kwenye orodha hiyo kutokana na ushindani mkubwa uliopo nchini.
"Nawashukuru sana walimu wangu, wazazi wangu na marafiki wote kwa kunitia moyo na kunipa ushirikiano katika masomo yangu mpaka kufikia hapa nilipo," amesema mhitimu huyo wa kidato cha nne.
Imam ameeleza matarajio yake ni kuwa mhandisi wa ndege, hivyo ataendelea na masomo ya tahasusi ya PCM ili aweze kufikia malengo hayo.
Loi Kitundu kutoka Feza Girls ambaye ameingia kwenye 10 bora matokeo ya kidato cha pili
Amesema licha ya kutoka katika familia ya kawaida, alijituma katika masomo yake huku akimwomba Mungu ili kufaulu mtihani wake wa mwisho na kuendelea zaidi na masomo ya juu.
Kwa upande wake, Loi Kitundu amesema juhudi zake zimemwezesha kufanya vizuri kwenye masomo hayo na ataendelea kujiimarisha zaidi ili afanye vizuri kwenye mitihani iliyo mbele yake.
"Nawashukuru sana walimu wangu kwa kunipa msaada kila ninapohitaji, mazingira ya shule ni mazuri na wanafunzi tuna ushirikiano mkubwa," amesema msichana huyo ambaye sasa anaingia kidato cha tatu.
Mzazi wa Imam, Fatma Mogaeka amewashukuru walimu na wafanyakazi wote wa shule ya Feza kwa ushirikiano waliompa mwanaye na kumwezesha kuingia kwenye orodha ya 10 bora kitaifa.
"Sina maneno mazuri ya kuwashukuru walimu kwa matokeo haya mazuri ya mwanangu," amesema mzazi akionyesha kufurahia maisha.