Waliotajwa 2025 wasifumbiwe macho ndani ya CCM
KUNA usemi ‘hakuna aijuaye kesho’… hii ikiwa na maana kuwa maisha ya mwanadamu au kiumbe chochote ni kama fumbo ambalo daima mwenye kujua siri ya majaliwa yake ni muumba (Mungu) na si mwingine yeyote.
Nimeanza kwa usemi huo kutokana na kile kinachoendelea kujadiliwa kwa sasa katika mitandao mbalimbali mara baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kubainisha kuwa wapo baadhi ya watu wakiwemo wasaidizi wake, wameelekeza akili zao katika uchaguzi wa mwaka 2025 na hivyo kujikuta wakishindwa kutekeleza ipasavyo majukumu waliyonayo hivi sasa.
Awali akizungumza juzi wakati akipokea taarifa ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Covid-19, Ikulu ya Dar es Salaam, Rais Samia aliweka
wazi juu ya uwepo wa watu hao ambao licha ya kuwa muda bado haujafika, tayari akili zao wamezielekeza katika uchaguzi wa mwaka 2025, kitu ambacho si sahihi.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa mikoa na viongozi wengine kutoka ngazi mbalimbali, Rais Samia alisema anachotarajia kukifanya kwa sasa ni kuwapunguzia majukumu viongozi hao ili wapate fursa nzuri ya kujipanga kwa ajili ya uchaguzi huo.
Binafsi naliona hili kama usaliti mkubwa au ‘kiherehere’ kinachoendana na uchu wa madaraka kutoka kwa watu hao kutokana na ukweli kuwa umepita takribani mwaka mmoja tu tangu nchi itoke katika uchaguzi, iweje leo hii ambapo kuna zaidi ya miaka mitatu mbele mtu aanze kuonesha tamaa ya kuwania madaraka.
Kwa kauli yake mkuu wa nchi, viongozi hao badala ya kumsaidia katika juhudi zake za kuwaletea maendeleo Watanzania, wao wamejielekeza miaka mitatu mbele bila kuzingatia msemo wa ‘hakuna ajuaye kesho’.
Napata mashaka na watu hawa. Machoni huonekana kama wapo karibu yako hali ya kuwa mioyoni mwao wamebeba ajenda zao na ndipo hapa unapata maana halisi ya usemi usemao umdhaniaye ndiye, siye. Hivyo kuna haja ya chama kuwamulika kwa nguvu zote watu hawa kwa kuwa tayari wameonesha ‘uchu’ wa madaraka.
Jambo la msingi ni vyema wakatambua kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa muda wa miaka mitano kufanyika kwa uchaguzi mkuu.
Halikadhalika Chama Cha Mapinduzi (CCM) chenyewe kimejiwekea awamu mbili za miaka mitano kwa mwenyekiti wa chama hicho pale anapoongoza nchi kama Rais kuendelea na jukumu hilo. Inapojitokeza
mwingine ndani ya chama akatolea jicho nafasi hiyo ni wazi kuwa suala hilo ni usaliti.
Katika hili naona umefika wakati kwa chama hicho tawala kuona haja ya kuwafuatilia kwa undani wanachama wake wote ambao tayari akili zao wamezielekeza katika uchaguzi wa 2025 kwa ajili ya kulinda maslahi mapana ya chama hicho kwa kuwa wanaweza kukisababishia mpasuko. Maana wahenga wanasema, “Mchelea mwana kulia, hulia mwenyewe’.
Hata hivyo, naamini CCM ina mkono mrefu na jicho la mbali kuwabaini watu hao waliotajwa na Rais Samia.
Hivyo uamuzi wa nini wafanye upo juu yao wakitambua kuwa kuendelea kuwafumbia macho ni sawa na kupandikiza kirusi ambacho mwisho wake, kitageuka na kuwaletea madhara wao wenyewe.