Maelezo ya picha,
Zaida Catalan alikwenda DR Congo kuchunguza uhalifu kwa ajili ya Umoja wa Mataifa pamoja na Michael Sharp (picha ya 2009)
Makumi ya wanamgambo wamehukumiwa kifo katika Jamuhuri ya Kidenokrasi ya Kongo kwa kuhusika katika mauaji ya wataalamu wawili wa Umoja wa Mataifa.
Wataalamu hao Zaida Catalan mwenye uraia wa Sweden na Chile na Mmarekani Michael Sharp walitekwa na kuuawa katika jimbo la Kasai mwaka 2017.
Walikuwa wakichunguza madai ya kuwepo kwa makaburi ya pamoja baada ya kuibuka kwa mapigano baina ya vikosi vya serikali na kikundi cha wanamgambo.
Mkalimani wao, Betu Tshintela,pia aliuawa. Miili yao ilipatikana siku 16 baada ya kutekwa nyara. Catalan alikuwa amekatwa kichwa.
Umoja wa Mataifa ulishitushwa na mauaji hayo na wakati huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alisema kuwa Umoja huo "ungefanya kila liwezekanalo kuhakikisha haki itendeka".
Hukumu zilizowatia hatiani washitakiwa zilitolewa na mahakama ya kijeshi katika mwisho wa kesi iliyodumu kwa miaka minne.
Kati ya makumi ya washitakiwa, 51, wakiwa ni karibu wanamgambo, walihukumiwa kifo. Lakini kutokana na kwamba Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo imekwisha tangaza usitishwaji wautekelezwaji wa hukumu ya kifo, hukumu hizi huenda zikaishia kuwa kifungo cha maisha gerezani.
Walikabiliwa na mashitaka mbali mbali, kuanzia ugaidi na mauaji na kitendo cha uhalifu wa kivita kwa kukata viungo, limeripoti shirika la habari la AFP.
Kanali Jean de Dieu Mambweni, aliyehukumiwa kifungo cha miaka 10 jela, alihukumiwa kwa kukiuka maagizo. Wengine wawili- mwandishi wa habari na afisa wa polisi waliachiliwa huru.
Zaidi ya vikao 100 vya mahakama vilikaa tangu kesi hiyo ilipoanza kusikizwa Juni 15, 2017 dhidi ya washukiwa waliotuhumiwa kwa mauaji ya wataalamu hao wa Umoja wa Mataifa.