Wanafunzi Walionusurika Ajali ya Lucky Vincent wafanya maajabu kidato cha IV



WANAFUNZI watatu walionusurika kwenye ajali ya Shule ya Lucky Vincent, wamefanya maajabu katika mtihani wa kidato cha nne na kufaulu vizuri kwenye masomo ya sayansi.

Wanafunzi hao ni Doreen Elibariki ambaye amepata daraja la pili, Wilson Godfrey (daraja la kwanza) na Sadia Awadh (daraja la pili).

Akizungumza kwa furaha kwa njia ya simu ya kiganjani, mzazi wa Sadia, Zaituni Abdul, alisema katika matokeo hayo anamshukuru Mungu kuwapigania watoto wao.

"Hakika namshukuru sana Mungu maana kwa matatizo waliyopitia hawa watoto sikutegemea kama watapata matokeo haya, hakika furaha yangu kubwa sana," alisema.

Alisema mwanawe ndoto yake kubwa ni kuwa daktari wa binadamu au rubani.


Mama mzazi wa Doreen, Neema Mshana, alisema alipopata matokeo hayo alimuona Mungu akimshika mkono mwanawe na wenzake.

"Hakika Mungu mwema anajua waja wake na hajawaacha, naamini ataendelea kutembea na watoto hawa mpaka watakapofikia ndoto zao," alisema.

Mwalimu wa darasa wa wanafunzi hao, Pascal Safari, aliwapongeza watoto hao kupata ufaulu mzuri licha ya matatizo waliyopitia.


Alisema katika darasa lao walikuwa jumla ya wanafunzi 65 ambao kati yao 26 wamepata daraja la kwanza akiwamo Wilson, 30 walipata daraja la pili akiwamo Doreen na mwenzake Sadia.

Pascal alisema wanafunzi wengine nane walipata daraja la tatu na mmoja daraja la nne.

Alisema watoto hao ambao manusura ya ajali wote walikuwa mkondo wa sayansi na wamefaulu vizuri.

"Naamini watoto hawa wanaweza kurudi hapa shuleni kuendelea na masomo yao ya kidato cha tano na sita kwani mazingira yaliyoko mazuri yanawafaa kuendelea na masomo," alisema.


Wanafunzi hao walipata ajali ya gari Mei 6, mwaka 2017, wakati wakielekea kwenye Shule ya Tumaini Junior iliyoko wilayani Karatu kwa ajili ya kufanya mtihani wa kujipima.

Katika ajali hiyo wanafunzi 32, walimu wawili na dereva walifariki papo hapo eneo la Rhotia wilayani Karatu, huku wanafunzi hao watatu wakinusurika.

Baada ya ajali hiyo Shirika lisilo la kiserikali la STEMM chini ya mratibu wa safari hiyo, Lazaro Nyalandu, liliwasiliana na Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo nchini Marekani, Steve Meyer, ambaye kwa ushirikiano na serikali waliwezesha kupatikana kwa hati ya kusafiria haraka kwenda nchini Marekani kwa matibabu zaidi baada ya kugundulika kuvunjika mara 36 mwilini mwao kila mmoja.

Doreen alilazimika kupelekwa kituo maarufu duniani cha Madona nchini Marekani, kutokana na tatizo la uti wa mgongo.


Agosti 18, mwaka 2017 walirejea nchini kwa msaada wa Shirika la Ndege la Mfuko wa Msamaria la Marekani linaloendeshwa na Frankline Graham, mtoto wa mwimbaji maarufu duniani, Bill Graham, wakiwa wameambatana na wazazi wao watatu na daktari bingwa wa mifupa wa Hospitali ya Mount Meru, Elias Mashalla na Dk. Siniphorosa Silalye.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad