WANAJESHI wa Tanzania wanaodumisha amani katika Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) chini ya Vikosi vya Umoja wa Mataifa (MINUSCA), walijeruhiwa baada ya gari walilokuwa wameabiri kukanyaga bomu.
Baada ya kulemewa na majeshi ya serikali na kutimuliwa katika miji muhimu, waasi sasa wamekuwa wakitumia mbinu ya kutega vilipuzi njiani.
Wanajeshi hao wa Tanzania walikuwa katika msafara wa magari ya MINUSCA yaliyokuwa yakitoka eneo la Berberati kabla ya gari walilokuwemo kukanyaga bomu.
Mmoja wa wanajeshi hao alijeruhiwa vibaya na alikimbizwa mjini Bangui kwa matibabu.
‘Hii ni mara ya tatu kwa wanajeshi wa MINUSCA kukanyaga vilipuzi vilivyotegwa na wanamgambo wa makundi ya waasi,’ ikasema taarifa ya Umoja wa Mataifa.
CAR ambayo ina takribani watu 5 milioni, ni miongoni mwa mataifa maskini zaidi ulimwenguni.
Rais Faustin-Archange Touadera alichaguliwa tena mwaka 2021 na anashikilia kuwa wanajeshi wake wanadhibiti asilimia 90 ya nchi.