Dodoma. Baada ya kiti cha Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa wazi, wana-CCM kadhaa, wakiwamo wabunge wanne wanatajwa kuwa na uwezekano wa kushika nafasi hiyo.
Mbali na wana-CCM hao, vyama vingine bado havijatoa msimamo wao kama watasimamisha mgombea katika uchaguzi wa Spika mpya.
Majina yanayotajwa ni wabunge, George Simbachawene (Kibakwe), Dk Pius Chaya (Manyoni Mashariki), Najma Giga (Viti Maalum) na Dk Tulia Ackson (Mbeya Mjini).
Dk Tulia kwa sasa ndiye Naibu Spika wa mhimili huo, huku makada wengine wa CCM wanaotajwa ni Dk Emmanuel Nchimbi na Abdulrahman Kinana.
Majina yanayotajwa CCM
Mbunge wa Manyoni Mashariki, Dk Pius Chaya ni mmoja wa wanaotajwa kuwa wanaweza kufaa kugombea nafasi hiyo.
Dk Chaya pia ni makamu mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii aliyezaliwa Desemba 5, 1976. Shahada yake ya uzamivu ya sera na mipango aliipata Chuo Kikuu cha Dodoma mwaka 2013.
Amefanya kazi shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (Unicef), Shirika la Utafiti na Tiba Afrika ( AMREF) na mhadhiri Chuo cha Mipango Dodoma na ameshika nafasi mbalimbali za uongozi.
Dk Tulia Ackson ni Naibu Spika wa Bunge aliyeanza kutumikia nafasi hiyo katika Bunge la 11 mwaka 2015, ikiwa ni miezi kadhaa baada ya kuteuliwa kuwa mbunge kupitia uteuzi wa Rais.
Hata hivyo, katika uchaguzi Mkuu wa 2020, aliamua kugombea jimbo la Mbeya mjini na kushinda, kabla ya kutetea nafasi yake ya Naibu Spika.
Aliwahi kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Alizaliwa miaka 45 iliyopita wilayani Rungwe mkoani Mbeya. Ana Shahada ya Uzamivu katika Falsafa kutoka Chuo Kikuu cha Cape Town nchini Afrika ya Kusini.
Mbunge wa Kibakwe na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, naye anatajwa kushika nafasi hiyo.
Simbachawene, aliyezaliwa Julai 5, 1968 amedumu bungeni kwa miaka 16 tangu achaguliwe kuwa mbunge wa Kibakwe mwaka 2005. Ameshika nafasi mbalimbali za uongozi, ikiwemo uwaziri.
Mwaka 2001 hadi 2005 alijiunga na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), alikotunukiwa shahada ya kwanza ya sheria.
Ameshiriki mafunzo ya kazi na taratibu za uendeshaji wa kamati za kibunge kwenye Bunge la Westminister na kutunukiwa cheti na mwaka 2010 alitunukiwa cheti kingine baada ya kuhitimu mafunzo juu ya bunge hilo.
Uzoefu wa Simbachawene unaweza kuwekwa kwenye makundi manne, kwanza ni uzoefu wa kazi za kitaalamu, pili ni kazi za kibunge, tatu ni uzoefu wa kazi za uwaziri na mwisho ni uzoefu wa utendaji ndani ya CCM.
Mbunge mwingine ni Mussa Azzan Zungu, aliyezaliwa Mei 25, 1952. Amekuwa mbunge wa jimbo la Ilala tangu mwaka 2005 na amewahi kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).
Bungeni alichaguliwa kuwa naibu mwenyekiti wa kamati ya mambo ya nje 2007-2011, mwenyekiti wa Umoja wa Wabunge wa Jumuiya ya Madola Tanzania na naibu mwenyekiti wa kamati wa Huduma za Jamii 2015 - 2018- 2012 na 2016 alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa Bunge.
Mwaka 1969 alijiunga na chama cha TANU akawa kiongozi kwenye tawi la chama shuleni.
Baadaye alihamia Toronto nchini Canada aliposoma stashahada ya ufundi wa vyombo vya anga pamoja na urubani. Baada ya masomo alifanya kazi ya uhandisi wa ndege nchini Canada hadi 1982.
1983 alipata nafasi ya kazi Falme za Kiarabu hadi 1993 aliporudi Tanzania.
Mwaka 2000 alirudi katika siasa akachaguliwa kuwa diwani wa CCM kwenye Kata ya Mchikichini na kuingia katika Halmashauri ya Ilala, Dar es Salaam.
Naye, Najma Murtaza Giga, aliyezaliwa Septemba 5, 1967 ni mbunge wa viti maalumu tangu mwaka 2015.
Najma ni mhitimu wa shahada ya kwanza ya sheria kutoka katika Chuo Kikuu Huria 2006.
Alikuwa miongoni mwa viongozi katika Jumuiya ya Wazazi ya CCM na mjumbe wa baraza kuu la jumuiya hiyo.
Tangu alipoingia bungeni mwaka 2015, amekuwa mmoja wa wenyeviti wa Bunge kwa ajili ya kumsaidia Spika, akiwa mwanamke wa kwanza kukalia kiti hicho kutoka upande wa Zanzibar.
Nje ya wabunge
Nje ya wabunge anayetajwa ni Dk Emmanuel Nchimbi, aliyezaliwa Desemba 24, 1971. Amewahi kuwa mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM, mbunge wa jimbo la Songea Mjini. Alishika pia nafasi kadhaa za uwaziri.
Alijiunga katika Chuo cha Mzumbe na kuhitimu Stashahada ya Juu ya Utawala (mwaka 1994 – 1997).
Wakati anahitimu Mzumbe, pia alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) na mwaka uliofuatia (1998), alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM).
Alisoma shahada ya uzamili ya usimamizi wa biashara Chuo Kikuu cha Mzumbe mwaka 2001 – 2003 akibobea kwenye maeneo ya (benki na fedha).
Dk Nchimbi aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Bunda (mwaka 2003 – 2005) na mwaka 2008 – 2011, alisoma na kufanikiwa kuhitimu shahada ya uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Mzumbe.
Mwaka 2005 alichaguliwa kuwa mbunge wa Songea Mjini na aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo.
Alidumu kwenye wizara hiyo hadi Oktoba 2006 alipohamishiwa kwenye Wizara ya Kazi, Ajira na Vijana, kisha Wizara ya Ulinzi na Kujenga Taifa ambako pia alikuwa Naibu Waziri hadi Novemba 2010.
Mei 2012 alihamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani kabla ya kujiuzulu Desemba 2013. Baadaye aliteuliwa kuwa balozi wa Tanzania nchini Brazil.
Kada mwingine wa CCM anayetajwa ni Abdulrahman Kinana.
Huyu ni Katibu Mkuu mstaafu wa chama hicho aliyekiongoza kuanzia 2012 hadi 2018. Alizaliwa mwaka 1952. Pia, amewahi kuwa Spika wa Bunge la Afrika Mashariki kuanzia 2001 hadi 2006.
Kinana ni mwanasiasa aliyeshika nyadhifa mbalimbali serikalini. Alihitimu shahada yake katika Chuo Kikuu cha Havard nchini Marekani, akibobea kwenye masuala ya mikakati.
Alikuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa, Naibu waziri wa Mambo ya nje na Uhusiano wa Kimataifa na Waziri wa Ulinzi.
Kinana aliwahi kufanya kazi na Jeshi la Wananchi la Tanzania kwa miaka 20 kabla ya kustaafu akiwa na cheo cha kanali mwaka 1972.
Abdulrahman Kinana pia aliwahi kuwa Spika wa Bunge la Afrika mashariki mwaka 2001 mpaka mwaka 2006.
Pia, aliwahi kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia tiketi ya CCM jimbo la Arusha kwa muda wa miaka 10.
Maoni ya wadau
Msomi wa shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Dodoma, Martin Lissu akizungumza na gazeti hili kuhusu anayefaa kushika nafasi hiyo, alisema Mkoa wa Singida una waziri mmoja, ni muhimu chama kikatoa nafasi kwa mkoa huo.
Grace John ambaye ni mfanyabiashara wa maduka ya jumla jijini Dodoma, alisema kwa kuwa nafasi hiyo inaweza kugombewa na mtu yeyote nje ya Bunge mwenye sifa, ni vema vyama vya upinzani vikajipanga kwa kuwashawishi wabunge wa CCM wawapigie kura.
Alisema ni wakati sasa kwa Bunge kupata Spika anayetoka nje ya mfumo wa wabunge ili kuleta mijadala iliyochangamka na yenye kujenga.
Sharifa Mohamed, aliyesema yeye ni kada wa CCM mkoani hapa alisema anatamani Spika wa sasa awe mwanamke kwa kuwa kati ya maspika sita ni mmoja ndiye alikuwa mwanamke, Anne makinda.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kupitia Mkoa wa Singida, Yohana Msita alisema chama kina makada wengi wa kugombea nafasi hiyo, lakini kwa upande wake anaona ni bora nafasi hiyo ikaendelea kuwa kwenye mikoa ya Kanda ya Kati, Dodoma na Singida.
Alisema kwa kuwa aliyejiuzulu alikuwa bado hajamaliza kipindi chake cha miaka mitano, Dodoma na Singida bado ina nafasi ya kutoa Spika wa Bunge.