Wanaotumika kumchafua Mkuu wa Majeshi waonywa

 


Siku za hivi karibuni kumekuwepo na taarifa za kupotosha ambazo zimekusudia kuwahadaa Watanzania kupitia mitandao ya Kijamii hususan YouTube, kwamba Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Salvatory Mabeyo anaingilia kati sakata la Rais na Spika jambo ambalo siyo la kweli.


Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limewataka wananchi kuzipuuza taarifa zilizowekwa kwenye mtandao huo kupitia kwenye channel inayojiita NEWS 24 zenye kichwa cha habari ‘‘KIMENUKA MKUU WA MAJESHI MABEYO ATOA AMRI NZITO KUJIUZULU KWA NDUGAI’’ na ‘‘MKUU WA MAJESHI MABEYO AINGILIA KATI SAKATA LA RAIS NA SPIKA’’.  Ukweli ni kwamba, kikundi cha watu wachochezi kimetoa taarifa za uongo na uzushi kwa kutumia sauti isiyo ya Mkuu wa Majeshi huku wakiwaaminisha Umma kuwa ni sauti ya Jenerali Mabeyo kwamba aingilia kati sakata la Spika.


JWTZ linawaomba Umma wa Watanzania kutoziamini taarifa hizo na wazipuuze kwa kuwa ni taarifa za uzushi na uchochezi zinazotungwa na kusambazwa na kikundi cha watu wasioitakia mema nchi kwa maslahi yao binafsi.


 Mkuu wa Majeshi hajatoa taarifa yoyote kuhusiana na yaliyozushwa kwenye mitandao kwa kuwa JWTZ halijihusishi kwa njia yoyote ile na masuala ya kisiasa na kamwe halitafanya hivyo.

JWTZ linatoa onyo kwa wale wote wanaotumika kumchafua Mkuu wa Majeshi, kwa lengo la kutaka kuliingiza Jeshi kwenye siasa.


Watu hao hawatafumbiwa macho na pindi watakapobainika hatua kali zitachukuliwa dhidi yao ili liwe fundisho kwa wengine.


Tunawaomba watanzania wote kuungana kwa kuendelea kupuuza na kukemea vikali taarifa hizo ambazo hazilitakii mema Taifa letu.

Nitumie fursa hii kuwahakikishia Watanzania wote kwamba JWTZ lipo imara, linaendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi na kwa mujibu wa Katiba kulinda na kuimarisha mipaka ya nchi yetu. Aidha, JWTZ linatekeleza majukumu yake ya msingi na lina mipaka yake kama yalivyoainishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad