Wasanii wa Kutazamwa Zaidi Bongo 2022

 


NI jambo la kawaida kuona kila mwaka wasanii wapya huingia kwenye gemu la muziki wa Bongo Fleva kisha kuanza kujitengenezea mashabiki ambayo ndiyo kazi ngumu nay a msingi zaidi katika kutafuta kuwa mkubwa kimuziki.

Mwaka 2021 umepinduka na sasa tumo kwenye huu wa 2022 ni vyema tutakumbushana listi ya wasanii waliongia kwenye gemu mwaka jana na kufanya vema na sasa wanatazamwa zaidi wakitarajiwa kukiwasha kwelikweli.

Kuingia kwenye gemu inaweza kuwa ni wasanii wapya kabisa ambao tumeanza kuwasikia kwa mara ya kwanza mwaka jana au wasanii ambao waliwahi kuwepo kwenye gemu, lakini umaarufu mkubwa wameupata mwaka jana na sasa wana kibarua cha kuthibitisha ubora wao;

ANJELLA

Angella au Black Angel kwa mara ya kwanza alisikika kitaifa mwezi Januari, 2021 baada ya kushirikishwa kwenye wimbo wa msanii na bosi wa Konde Gang, Harmonize.

Baada ya Anjella kuonesha kipaji kikubwa kwenye wimbo huo, mabosi wa lebo hiyo ya pili kwa ukubwa Tanzania waliamua kumsajili na kumfanya kuwa first lady wao; yaani msanii wa kike pekee ndani ya lebo.

Anjella kiukweli mwaka jana alifanikiwa kupata tuzo ya kwanza kutoka chaneli yake ya YouTube kwa kufikisha wafutiliaji (subscribers) 100,000.

Anjella ambaye alifanya vizuri na Ngoma ya Nobody alifikia mafanikio hayo ikiwa ni miezi mitatu tangu atangazwe rasmi kuwa chini ya lebo hiyo inayomilikiwa na Harmonize. Baada ya kusaini mkataba aliachia wimbo wake wa kwanza uitwao Kama aliomshirikisha Harmonize ukiwa ni wa pili kufanya pamoja.

Katika kuwashukuru mashabiki wake, Anjella alisema; “Haikuwa kazi rahisi tangu nimeianza safari yangu ya muziki rasmi, nimeuona upendo wenu wa dhati mashabiki wangu ambao mmejitolea muda wenu kufuatilia kazi zangu.”

Baada ya hapo aliachia ngoma yake binafsi ikifuatiwa na kutambulishwa rasmi kuwa msanii wa lebo hiyo katika bonge moja la pati ya kumkaribisha lililofanyika Makao Makuu ya Konde Gang, Mbezi-Beach jijini Dar.

Hadi sasa Anjella ameshaachia ngoma takriban tano zilizopata kutazamwa zaidi ya mara milioni 13 kwenye Mtandao wa YouTube. Huku akaunti yake ya Instagram ikisoma kuwa nusu milioni, yote ni kuonesha ni jinsi gani amejua kuingia kwenye gemu na sasa anatazamiwa kufanya vizuri mwaka huu.

LODY MUSIC

Anatajwa kama msanii pekee mpya aliyeingia kwenye gemu mwaka jana bila mgongo wa lebo kubwa tunazozijua kama zile za Diamond Platnumz, King Kiba au Harmonize wala kiki za kushindanishwa na wasanii ambao tayari wapo kwenye gemu.

Lody Music alianza kupenya taratibu kwenye gemu alipoachia ngoma yake ya Linapotea, hiyo ikiwa ni mwezi Mei, mwaka jana.

Lakini umaarufu zaidi aliupata alipoachia goma lake linalokwenda kwa jina la Kubali ambalo limefanya vizuri na bado linafanya poa hadi sasa.

Lody Music anatamba zaidi kwa aina yake ya muziki wa tofauti, muziki wa taratibu ambao wasanii wengi wa kisasa wanaukwepa, huku mashairi yake yakiwa yamelalia zaidi kwenye suala zima la mapenzi.

Kiukweli Lody Music ndiyo mpango mzima na inaonekana aliamua kuachia kazi za kufuatana. Msanii huyu alipoachia kazi yake inayojulikana kama Naenjoy, ulibamba, ni ngoma nyingine iliyozidisha umarufu wa msanii huyu kwani ilitrendi hapa na pale ambapo radio nyingi nchini Tanzania zilicheza ngoma hii.

Lord Music amebarikiwa na sauti nzuri na pia ana uwezo mkubwa mno wa kuandika nyimbo.

MAC VOICE

Mwezi Machi, 2021, msanii Rayvanny alizindua lebo yake ya Next Level Music na ilipofika Septemba akamtangaza msanii first born wa lebo hiyo anayeitwa Mac Voice.

Akiwa na miezi mitatu tu kwenye gemu, Mac Voice ameachia EP yenye ngoma kali nne na kujizolea umaarufu kwa namna yake.

Kingine kilichowagusa watu kuhusu yeye ni vile mashabiki wa Bongo Fleva wanavyomfananisha na Rayvanny kuanzia sauti, aina ya uimbaji, mtindo wa uandishi wa mashairi na hata mwonekano wake.

Licha ya upya wake kwenye gemu, Mac Voice anabebwa na namba kwani tayari ndani ya miezi hii mitatu tu amekusanya watazamaji zaidi ya milioni 5 kwenye chaneli yake ya YouTube na kumfanya kuwa msanii mpya mwenye watazamaji (views) wengi zaidi.

KUSAH

Pamoja na kwamba alisikika muda mrefu tangu akiwa na mpenzi wake ambaye ni msanii wa Bongo Fleva aitwaye Ruby na kutamba na ngoma kama vile Kodo, Chelewa, Kelele na nyinginezo, lakini mwaka jana ndiyo uliokuwa mwaka wa mafanikiwa zaidi.

Ngoma yake ya I Wish imemfanya kuwa juu zaidi huku akipata mashabiki wengi ambao wanamtazama zaidi kwa mwaka huu, wakiamini atakuwa moto wa kuotea mbali na kutoboa zaidi ya hapo alipo.

SARAPHINA

Huyu ni binti mwenye kipaji kikubwa ambaye pamoja na kuwa kwenye gemu la muziki tangu 2018, lakini mwaka jana ndipo milango ilipoanza kufunguka na sasa anatazamwa kama staa mwingine mkubwa wa kike wa Bongo Fleva ajaye.

Saraphina amesikika na bado ngoma zake zinapenya kama Kushki, Sitaki Tena, Pekecha na nyingine kibao.


ABBY CHAMS


Akiwa na umri wa miaka 18 tu, Abby Chams nyota yake inazidi kung’ara kunako gemu la Bongo Fleva. Abby Chams amesikika na bado anasika na ngoma kama Tucheze, Chapa Lapa na nyinginezo huku akiwa na madili mengi ya ubalozi.


MAKALA; ELVAN STAMBULI, BONGO

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad