Dar es Salaam. Wasichana wameng'ara zaidi kwenye orodha ya wanafunzi 10 bora kitaifa kwenye matokeo ya kidato cha nne yaliyotangazwa leo.
Hayo yamebainishwa leo Januari 15, 2022 mkoani hapa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Mitihani (Necta), Dk Charles Msonde wakati akitoa taarifa ya matokeo ya darasa la nne, kidato cha pili na kidato cha nne.
Matokeo hayo yanaonyesha wasichana wanane wameingia kwenye orodha ya wanafunzi kumi bora waliofanya vizuri kwenye matokeo ya mtihani wa kidato cha nne uliifanyika Novemba mwaka jana.
Kati ya hao, wasichana saba wanatoka shule ya St. Francis Girls iliyopo mkoani Mbeya, msichana mwingine akitoka shule ya Bright Future Girls huku wavulana pekee walioingia kwenye kumi bora kitaifa wakitoka shule za Feza Boys ya Dar es Salaam na Ilboru ya Arusha.
Walioingia kwenye orodha hiyo ni pamoja na Consolata Lubuva, Buthoi Nkangaza, Wilihelmina Mujarifu, Glory Mbele na Mary Ngoso, wote kutoka shule ya St. Francis Girls iliyopo mkoani Mbeya.
Wengine ni Holly Lyimo (Bright Future Girls), Blandina Chiwawa (St. Francis Girls), Imam Mogaeka (Feza Boys), Mfaume Madili (Ilboru) na Clara Assenga (St. Francis Girls).
Kwa upande wa shule 10 bora kitaifa, Dk Msonde amezitaja kuwa ni pamoja na Kemebos (Kagera), St. Francis Girls (Mbeya), Waja Boys (Geita), Bright Future Girls (Dar es Salaam) na Bethel Sabs Girls (Iringa).
Shule nyingine ni Maua Seminary (Kilimanjaro), Feza Boys (Dar), Previous Blood (Pwani), Feza Girls (Dar) na Mzumbe (Morogoro).