Watu 16 mbaroni madai kufukua, na kuiba mwili wa mtoto mdogo



​​​​​​​WATU 16 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Singida kwa mahojiano kutokana na kufukuliwa na kuibwa kwa mwili wa mtoto, Christian Samson, mwenye umri wa mwaka mmoja na mwezi mmoja.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Kamishna Msaidizi (ACP) Stella Mutabihirwa.
Inadaiwa kuwa mwili wa mtoto huyo ulifukuliwa kwa kile kilichoelezwa ni kutokana na imani za kishirikina.

Mtoto huyo alikuwa amezikwa kwenye makaburi ya Kipondoda yaliyoko kitongoji cha Kipindoda, tarafa na wilaya ya Manyoni.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Kamishna Msaidizi (ACP) Stella Mutabihirwa, katika taarifa yake jana kwa vyombo vya habari, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Alisema baada ya kupata taarifa hizo, jeshi hilo kupitia makachero wake lilifika katika eneo la tukio na kufanya uchunguzi wa awali na kujiridhisha kuwa ni kweli kaburi lilifukuliwa na mwili huo kuibwa huku jeneza likiachwa tupu.


 
Kamanda Mutabihirwa alisema Januari 18, mwaka huu, saa 1:15 asubuhi, Jeshi la Polisi lilipokea taarifa kuwa usiku wa kuamkia tarehe na mwezi huo, kwenye eneo la makaburi hayo, mwili wa marehemu, aliyekuwa mkazi wa Kipondoda ambaye alifariki Januari 15, mwaka huu, kwa maradhi na kuzikwa siku iliyofuata, ulifukuliwa na kuchukuliwa kutoka kwenye jeneza na watu wasiojulikana.

Alisema watu hao baada ya kufanya uhalifu huo, walitokomea kusikojulikana hadi  Jeshi la Polisi lilipopata taarifa na kutuma timu ya makachero ambao kwa kushirikiana na viongozi wa kijiji na raia wema, walifanya msako mkali.

Mutahibirwa alisema siku sita baada ya maziko, yaani Januari 21 majira ya saa 6:15 usiku, mwili wa marehemu ulipatikana ukielea kwenye kisima cha maji chenye urefu wa futi 12 kilichoko jirani na eneo la kata hiyo.


’’Jeshi la Polisi linawashikilia watuhumiwa 16 kwa mahojiano. Mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi wa kitabibu katika Hospitali ya Wilaya ya Manyoni na kukabidhiwa kwa ndugu kwa hatua za mazishi,’’ alisema Mutabihirwa.

Kamanda huyo aliwasihi wananchi kuachana na kujihusisha na imani za kishirikina na kutenda matendo mema yanayompendeza Mwenyezi Mungu kutokana na tukio kujionyesha dhahiri kuwa na viashiria vya moja kwa moja vya imani hizo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad