Polisi katika jimbo la Zamfaraaskazini-magharibi mwa Nigeria wamewakamata watu wanne wanaodaiwa kuhusika na ulaji nyama za watu na kuuza sehemu za binadamu, jambo ambalo ni nadra sana katika eneo hilo.
-
Kamishna wa polisi katika jimbo hilo Ayuba Elkanah aliwaambia waandishi wa habari katika mji mkuu Gusau siku ya Alhamisi kwamba washukiwa hao walikamatwa baada ya maafisa wa upelelezi kupata maiti katika jengo ambalo halijakamilika huku baadhi ya sehemu za mwili zikiwa zimetolewa, Ilikuwa ni katika harakati za kufanya uchunguzi wa kupotea kwa mvulana wa miaka tisa.
-
Washukiwa hao wakiwemo wanaume wawili na wavulana wawili walikamatwa wiki iliyopita, na washukiwa wengine wa genge hilo bado wanasakwa.
-
Kuhusika na uuzaji wa sehemu za binadamu na ulaji nyama si jambo la kawaida katika jimbo la Zamfara. Lakini ni moja wapo ya maeneo ya Nigeria yaliyokumbwa zaidi na wimbi la mauaji na utekaji nyara kwa ajili ya fidia na magenge yenye silaha huku mamlaka zikikabiliwa na ukosoaji kwa kushindwa kukabiliana na ghasia hizo.