JESHI la Polisi Mkoa wa Njombe, limetoa tahadhari kwa jamii kutoruhusu watoto wao kulala na watu wazima ili kuepuka kufanyiwa vitendo vya ukatili hasa wa kingono.
Kamanda wa Polisi mkoa njombe, Hamisi Issah.
Tahadhari hiyo ilitolewa na Kamanda wa Polisi mkoa huo, Hamisi Issah, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala mbalimbali yakiwamo pia yanayohusu watoto kulindwa.
"Tunasema kila siku kwamba watoto wadogo wanahitajika kulindwa na mnapokuwa mnawalaza usiku wasilale na watu wengine wakubwa ingawa ni wanafamilia, walale peke yao na watu wakubwa walale peke yao vinginevyo utakuta mtoto mdogo amefanyiwa ukatili," alitahadharisha Kamanda Issah.
Kwa mujibu wa Kamanda Issah, watoto wanapaswa kukaguliwa kila siku kuhakikisha wapo salama.
Alitoa rai kwa wazazi na walezi kutoruhusu watoto wao kutoka bila sababu ya msingi badala yake watulie nyumbani.
"Kwa kipindi hiki cha likizo wale wanaoruhusu watoto kwenda sehemu mbalimbali kutembea tafadhali achana na mtindo huo," alisisitiza Kamanda Issah.
Pia aliwakumbusha madereva wa magari na bodaboda kujua wajibu wao wawapo barabarani kwa kuangalia vivuko vya watoto na usalama wa watu wengine wanaoitumia barabara na kuepuka kufanya vitu kwa kuwakomoa watu au kwa kuwasababishia madhara mengine," alisema.