Waziri Majaliwa aonya watengeneza migogoro serikalini



WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa, amewataka watu wanaotengeneza migogoro dhidi ya viongozi wa Serikali, waache mara moja. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Waziri Majaliwa alitoa onyo hilo juzi, tarehe 31 Desemba 2021, akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Ruangwa, mkoani Lindi.

Waziri Majaliwa aliwataka watu hao wawaheshimu viongozi walioko madarakani, kwani uwepo wao ni mpango wa Mungu.

“Madaraka yote yanatolewa na Mungu,  amepanga kila kitu. Nani atakuwa nani katika kipindi gani,  hata ukilazimisha kutaka nafasi hiyo huwezi kama Mungu hajasema nenda na wala usitumie njia yoyote kumuathiri mwenzako ili apate madhara, eti atoke hapo ili uende hapo,” alisema Waziri Majaliwa.


 



Waziri Majaliwa alisema ” nani amekwambia utakwenda hapo? Nani amezungumza na Mungu? Tuache tabia ya kuacha viongozi kufanya kazi yao ya kuwahudumia Watanzania na kuwatengenezea migogoro kila siku,  tena mingine ya kusingizia tu.”

Waziri Majaliwa alisema kuwa, wanaotaka kukwamisha viongozi kutekeleza majukumi yao,  hawatafanikiwa.

“Kila nafasi imetengenezwa na Mungu na kila anayekwenda kuongoza Mungu ndiye amesema wewe utakuwa pale. Kama hajasema  hutakuwa, utatumia mihela  mingi itapotea tu,  utakwenda na mambo mengi ya giza  hutadumu. Tuheshimu waliokuwa katika nafasi ya kuwatumikia Watanzania,”


“Uongozi wa sekta yoyote ile unaongozwa na Mungu,  unaweza ukapambana sana ukitaka ukae ukakuta hukai anakaa mwingine,  kwa hiyo utaanza kuathiri wote wanaokaa hapo sababu wewe unataka, wakati Mungu hataki. Lazima tujue kwamba,  madaraka yoyote yanatolewa na Mungu,” alisema Waziri Majaliwa.




Waziri Majaliwa aliwaomba Watanzania wamuombee Rais Samia Suluhu Hassan, ili aendele kutekeleza majukumu yake ya kuiongoza nchi.

“Kwa bahati nzuri rais wetu amekuwa mtumishi serikalini,  anajua kwamba Watanzania wanatamani nini kukiona katika maeneo yao na nyie wote mnajua toka alipoingia madarakani nini amefanya mama mwenye busara na huruma.  Anajua nini anafanya. Watanzania jukumu letu  tuchape kazi sana, hatuna namna ya kumshukuru zaidi ya kuchapa kazi,” alisema Waziri Majaliwa na kuongeza:

“Tumejenga madarasa, tumejitahidi pia kusambaza vituo vya afya kwenye wilaya hii,  tena kimkakati ili watu huduma ya afya iwafuate huko huko. Wana Ruangwa mnataka nini?  Rais ndio huyu anayepitisha mafungu na kila tunachomwambia anasema peleka,  sababu anawapenda wananchi wote.”

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad