Waumini wa Kanisa la Kiadventista la Boigesa katika eneo la Bunge la Bobasi kaunti ya Kisii nchini Kenya walipigwa na bumbuwazi siku ya Jumamosi, Januari 8, baada ya kukuta kanisa lao limevunjwa na wezi walioamua kupika ndizi, wali na kuiba vifaa.
Mzee wa kanisa Tom Mosoba, alisema wezi hao walivunja kanisa hilo Jumatano usiku, wakapika ndizi, wakala na kuiba vyombo, mfuko mmoja wa mahindi, spika mbili, kipaza sauti na gitaa.
Mosoba aliwaelezea waandishi wa habari kuwa wezi hao walimsukuma mmoja wao kupitia kwenye mwanya uliopo paani huku wenzake wakitumia shoka kuvunja mlango.
Chifu wa eneo hilo Henry Mirera alisema mshukiwa mmoja wa tukio hilo ambaye ni mkazi wa Kenyenya alikamatwa na anazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Itumbe akitazamiwa kuhojiwa.
“Mshukiwa alinaswa katika eneo la tukio na amekabidhiwa kwa maafisa wa upelelezi wa makosa ya jinai kumchunguza, makanisa hayana walinzi. Kwa hiyo wazee wangekuwa wakisafirisha vifaa hivyo wakati wa siku za ibada na kuvirudisha nyumbani kwao,” alisema.
Visa vya wezi kuvunja kanisa vimekuwa vikikithiri siku za hivi karibuni nchini kenya ambapo wakazi wa kaunti ya Vihiga waliachwa na mshtuko baada ya watu wasiojulikana kuvamia Kanisa la Mumbita Church of God Luanda na kujisaidia haja kubwa ndani ya eneo la mchungaji.
Tukio hilo limelazimisha Church of GOD Afrika Mashariki (Kenya) kuandaa sherehe ya utakaso inayotarajiwa kufanyika Jumanne, Novemba 9, 2021, ili kufukuza pepo na kuweka wakfu tena wa kanisa la Mumbita.
Kulingana na mkurugenzi wa ustawi wa jamii katika mkutano mkuu wa kanisa hilo Wycliffe Ochieng, wezi hao pia waliiba lita 40 za rangi zilizokuwa zimehifadhiwa ndani ya kanisa hilo.